The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imetenga shilingi milioni 100 kufadhili wanafunzi 1000 watakaosoma elimu na mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vya VETA.
Ufadhili huo umetolewa chini ya mpango wa ‘NBC Wajibika Scholarship’ kupitia ushirikiano kati ya Benki hiyo na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Hafla ya utiaji saini makubaliano ya ushirikiano huo imefanyika jana tarehe 20 Julai, 2023 jijini Dodoma ambapo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) wamesaini mkataba wa Makubaliano ya ufadhili wa vijana hao.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa ufadhili huo unakwenda kutimiza azma ya Serikali ya kutoa Elimu na Mafunzo yatakayowawezesha vijana wa kitanzania kupata ujuzi wa kujiajiri ama kuajiriwa.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa mageuzi makubwa ya elimu yanayotarajiwa kutokea, yanatilia mkazo mafunzo ya ufundi stadi, hivyo Benki hiyo imekuja wakati muafaka kuiunga mkono Serikali katika mpango huo.
"Tumekuwa tukizungumza mafunzo ya ufundi stadi sana, tunataka tutoe elimu hiyo inayomwezesha kijana kuwa na ujuzi, leo Benki ya NBC imetushika mkono kwenda hatua moja zaidi ya kufanikisha azma hii," amesema Prof. Mkenda
Aidha Waziri Mkenda amewataka wadau wengine kuiunga mkono Serikali kwenye kuimarisha mafunzo na kuongeza fursa katika Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Vyuo vya Kati ili vijana wanufaike na ujuzi utakaopatikana.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NBC, Theobald Sabi amesema kupitia ushirikiano na Wizara,
vijana hao 1000 wataingizwa katika mpango maalum wa elimu ya Fedha unaojulikana kama NBC Business’ Club ambapo watafunguliwa akaunti maalum zitakazowawezesha kujiwekea akiba, bila gharama yoyote ya kibenki na kupata ushauri juu ya uwekezaji na kujipatia fursa ya kujijenga kiuchumi kupitia mikopo.
"Changamoto ya ajira kwa vijana ni kilio cha Dunia nzima, suluhisho thabiti ni kutengeneza mazingira bora kuwawezesha vijana kujiajiri au kujiendeleza kwa kuwa na ujuzi," amesema
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, ameishukuru Wizara kwa kuwezesha kupatikana ufadhili huo kutoka Benki ya NBC ambao utawezesha vyuo vya VETA kutoa Mafunzo ya Ujuzi kwa vijana wengi.
“Kwa hili walilofanya NBC, VETA tunakwenda kuhakikisha vijana wa kitanzania wanapata ujuzi mahiri na kuwafungulia fursa za ajira,” amesema.
CPA Kasore ameahidi kuwa VETA itazingatia maelekezo yaliyotolewa na kuhahakisha fedha zitakazotolewa zinatumika kwa uwazi na kunufaisha walengwa ili hatimaye kuleta matokeo yaliyokusudiwa.