The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Prof. Mchome ahimiza utatu katika kufikia malengo ya VETA
Posted on: Monday, 16 October 2023
Prof. Mchome ahimiza utatu katika kufikia malengo ya VETA
Kikao cha kwanza cha Bodi ya Tisa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VET Board)
kimehitimishwa, tarehe 14 Oktoba 2023, jijini Arusha, huku Mwenyekiti wa Bodi
hiyo, Profesa Sifuni Mchome akihimiza utatu wa Bodi, Menejimenti na Watumishi katika
kutekeleza majukumu ya VETA.
Katika kikao hicho kilichofanyika kwenye Chuo cha VETA cha Hoteli na Utalii, Njiro, jijini
Arusha, Profesa Mchome amesema kuwa Bodi inatakiwa kutoa maelekezo sahihi,
Menejimenti ya VETA kuanda miongozo na kuweka mikakati thabiti ya utekelezaji na
wafanyakazi kujitoa kwa dhati katika kutekeleza majukumu mbalimbali.
“Sisi tunachotaka ni kufanya kazi kwa utatu ili kufikia malengo…Katika utatu huo,
Watumishi wasiiangushe Menejimenti, Menejimenti isiiangushe Bodi na Bodi itatoa
maelekezo sahihi ya kitu cha kufanya… ule utatu ukitimia basi tutaweza kufikia
malengo”, amesema.
Ameitaka Menejimenti ya VETA kutambua na kuichambua miradi ya Kimkakati
iliyopangwa au inayotekelezwa na Serikali, kisha kubuni programu mbalimbali za
mafunzo ili kujibu mahitaji ya ujuzi katika miradi hiyo.
Prof. Mchome amesema miongoni mwa mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita ni
kuwapatia wananchi ujuzi ambao ndiyo msingi mkuu katika kuwawezesha kushiriki
katika uchumi wa sasa wa dunia na kusisitiza kuwa VETA inategemewa zaidi katika
kufanikisha mkakati huo.
“Nchi inahitaji ujuzi unaoendana na maendeleo ya kidunia na VETA ndiyo chombo cha
kubaini na kutekeleza mahitaji hayo,” amesema.
Akizungumzia Sera mpya ya Elimu na mabadiliko katika mitaala ya Elimu, Profesa
Mchome amesema, VETA inategemewa kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa
mitaala mipya ya sekondari, kwani mwelekeo wa mitaala hiyo ni mafunzo ya ujuzi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore ameishukuru Bodi mpya kwa
kuanza vyema katika kupanga utekelezaji wa majukumu yake na kuahidi kwa niaba ya
Menejimenti ya VETA kutekeleza maelekezo na miongozo mbalimbali itakayotolewa na
Bodi.
Bodi ya Tisa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi inayowahusisha wajumbe kutoka
taasisi za Serikali, sekta binafsi, waajiri, waajiriwa na taasisi za dini ilianza kikao chake
kwa kufanya kikao kazi cha kueleweshana na kujengeana uwezo kuhusu utekelezaji wa
majukumu mbalimbali ya Mamlaka.