The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Prof. Mchome awataka wahitimu wa ufundi stadi waunde vikundi
Posted on: Sunday, 10 March 2024
Prof. Mchome awataka wahitimu wa ufundi stadi waunde vikundi
Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Prof. Sifuni Ernest Mchome ametoa wito kwa vijana wanaopata mafunzo kwenye vyuo vya VETA hapa nchini kuweka utaratibu wa kufanya kazi kwa pamoja kupitia vikundi na kwenda katika sehemu mbalimbali za nchi kufanya kazi walizofundishwa wakiwa pamoja, kwa kuwa kuna uwezekano wa kufanya mambo makubwa.
Prof. Mchome ametoa wito huo juzi, tarehe 8 Machi, 2024, katika chuo cha VETA Wilaya ya Karagwe, wakati wa kuhitimisha ziara ya Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi katika Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera na Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Karagwe, mkoani Kagera.
” Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, viijana mkijiunga kwa pamoja, uwezekano wa kufanya mambo makubwa ni mkubwa na uwezekano wa kupata misaada kutoka sehemu mbalimbali, hasa Serikalini ni mkubwa,” amesema.
Amesema VETA inatoa fursa kwa vijana kuweza kujifunza ujuzi unaowawezesha kujiajiri wenyewe na pia kuweza kupata fursa za kuajiriwa na kwamba kuna fursa nyingi ambazo wananchi, hasa vijana wanaweza kuzitumia kwa ajili ya kupata mafunzo ya aina mbalimbali yanayogusa maendeleo ya nchi na maisha yao kwa ujumla.
“Tunamshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi kubwa ambazo ameweka katika ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi hapa nchini, hizi juhudi tutazisimamia na tutahakikisha yale yote yaliyopangwa yanajitokeza katika ubora wake ili yalete ufanisi katika Elimu na mafunzo ya Ufundi stadi,” amesema.
Ameongeza kuwa miongoni mwa kazi kubwa ni ya kuhamasisha vijana kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi, na baada ya kupata mafunzo wawe na utaratibu wa kufanya kazi kwa pamoja katika vikundi.
Ametumia fursa hiyo pia kuwahamasisha vijana wanaohitimu vyuo vya elimu ya juu kujiunga na vyuo vya VETA ili kupata kitu cha ziada kinachoweza kuwasaidia kuajirika kwa urahisi.
Ziara ya Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ilikuwa na lengo la kujionea namna vyuo hivyo vinavyotoa mafunzo na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vya VETA.