The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe amewakumbusha watendaji wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuwa Uongozi wa nchi una mategemeo makubwa kwa taasisi hiyo katika kusaidia kubadilisha uchumi wa nchi na kupunguza tatizo la ajira, kupitia mafunzo ambayo yanawapa wananchi, hasa vijana, ujuzi unaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa, hivyo kuongeza tija katika uzalishaji.
Prof. James Mdoe ameyasema hayo, tarehe 9 Mei 2022, jijini Dodoma, wakati akizungumza na watendaji wa VETA katika kikao kilichowahusisha Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo vya VETA Makao Makuu, Wakurugenzi wa Kanda za VETA na Wakuu wa Vyuo vya VETA nchini kote.
“Mnasikia kila mara Mheshimiwa Rais akizungumzia ujuzi ujuzi, na katika mazungumzo hayo hakosi kuitaja VETA. Naomba mlifahamu hilo na mkilala, mkiamka mlijue hilo na kulifanyia kazi kwa uzito,” alisema.
Aliwaomba kufanya kazi kwa bidii na kuendelea kukabiliana na changamoto walizonazo.
“tunajua changamoto za uhaba wa watendaji na (Wizara) tunalifanyia kazi na tuna imani tutaendelea kupata wafanyakazi zaidi kwa ajili ya kuendesha mafunzo,” aliongeza.
Sambamba na hilo, Prof. Mdoe aliwaomba kulibeba kwa uzito mkubwa jukumu la ukamilishaji wa ujenzi wa vyuo vipya vya VETA baada ya kupata fedha za UVIKO 19, kwani kazi hiyo ni ya kipaumbele kikubwa kwa Serikali.
Katika maneno ya utangulizi, Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dkt. Noel Mbonde alisema shughuli ya ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vya wilaya ina tarehe mahsusi za ukamilishaji, ambapo tarehe ya mwisho ya Wizara ni 30 Mei 2022, hivyo akaiomba VETA ikamilishe mapema zaidi ya tarehe hiyo ili Wizara nayo iweze kupata fursa ya kufanya majumuisho ya taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa upande wake.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, kwa niaba ya watendaji wa VETA aliahidi kuzingatia maelekezo na nasaha za viongozi wa Wizara na kusema kuwa wamejipanga kukamilisha mradi wa ujenzi wa vyuo vipya vya wilaya kwa wakati.