The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Serikali ya Awamu ya Sita: Kipaumbele ni wananchi kupata ujuzi
Posted on: Friday, 25 March 2022
Yawezesha vyuo 29 vya ufundi stadi vya wilaya, 4 vya mikoa kujengwa
Yafadhili mafunzo ya uanagenzi kwa vijana 14,440
Moja ya vipaumbele vikubwa vya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kujengea ujuzi wananchi wake, hasa vijana. Imani kubwa ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwa ujuzi ndio utakaowezesha kuwa na rasilimali watu yenye kuongeza tija katika uzalishaji, kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, kuwawezesha wananchi mmoja mmoja kujikwamua kiuchumi na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla. Mhe. Rais, pamoja na viongozi wengine wa kitaifa wamekuwa wakizungumza mara kwa mara kusisitiza juu ya kipaumbele hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) anaeleza kuwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha kwa vitendo kuwa serikali yake inataka kuona vijana wanapata ujuzi. Kwa shauku na matakwa hayo, Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayohusu elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
“Miongoni mwa ushahidi wa utashi na nia ya dhati ya Serikali katika kuendeleza ujuzi ni uendelezaji wa ujenzi wa vyuo 29 vya ufundi stadi vya ngazi ya wilaya, ambapo kati ya hivyo, vyuo 25 vinajengwa na VETA kwa utaratibu wa kutumia nguvukazi ya ndani, yaani “Force Account” na vinne vinajengwa na Halmashauri husika kwa usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Katika kipindi chote cha mwaka mmoja wa uongozi wa Mhe. Samia, serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyuo hivyo” anasema Mkurugenzi Mkuu.
Mkurugenzi Mkuu anaendelea kusema kuwa msukumo zaidi umeoneshwa katika Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 ambapo serikali ilitoa Shilingi Bilioni 48.5 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa vyuo 25 vya ngazi ya Wilaya, vinne (4) vya ngazi ya Mkoa na Mabweni mawili ya Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC).
Anasema kuwa vyuo vingi viko katika hatua za mwisho za mwisho za ukamilishaji. Matarajio ni kwamba hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu, vyuo vyote vitakuwa vimekamilika tayari kwa kuanza kutoa mafunzo.
“Katika juhudi za kujenga ujuzi kwa wananchi, serikali haijaishia kwenye ujenzi wa vyuo na miundombinu ya mafunzo pekee, bali pia kuandaa na kutekeleza programu za kuwezesha makundi mbalimbali kupata fursa za mafunzo ya ufundi stadi ili wawe na ujuzi wa kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi,” anaongeza Mkurugenzi Mkuu.
Anautaja Mpango wa Mafunzo ya Uanagenzi kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, kuwa umechangia kwa kiasi kikubwa sana kuwezesha vijana wengi kupata fursa za elimu na mafunzo ya ufundi stadi. Kupitia mpango huu, jumla ya vijana 14,440 walinufaika na mafunzo kwenye vyuo 72 vya Ufundi Stadi nchini, kati yao, vijana 7,538 walidahiliwa katika vyuo 32 vya VETA. Mafunzo kwa ngazi ya vyuo yalikamilika mwezi Desemba, 2021, kisha wanafunzi hao wakaenda kwenye mazoezi ya vitendo sehemu za kazi (viwandani). Anasema kuwa vijana wengi wametoa ushuhuda wa namna mpango huo ulivyobadilisha maisha yao.
Mkurugenzi Mkuu anataja zoezi lingine lililofanyika kwa lengo la kuwezesha vijana kujiajiri au kuajiriwa ni la kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo ambapo jumla ya vijana 2,537 wamerasimishwa ujuzi wao na kutunukiwa vyeti. Zoezi hilo limefadhiliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Mkurugenzi Mkuu anasema kuwa vyeti hivyo vinawawezesha mafundi ambao hawakupitia mafunzo rasmi kujiendeleza kielimu, kuboresha huduma wanazotoa, kufungua makampuni yao, kupata zabuni mbalimbali pamoja na kupata fursa za mikopo kwenye taasisi mbalimbali za fedha.
Mkurugenzi Mkuu anasema kuwa VETA inapokea kwa uzito mkubwa kipaumbele hicho cha Serikali na kwamba ikiwa ndiyo chombo kilichopewa dhamana ya uendeshaji elimu na mafunzo ya ufundi stadi, inaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuimarisha ubora wa mafunzo hayo.
Anataja miongoni mwa jitihada hizo kuwa ni ununuzi wa mitambo, zana na vifaa vingine vya kufundishia na kujifunzia, ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, VETA imetekeleza manunuzi ya mitambo na zana za kufundishia zenye thamani ya Sh. Bilioni 5.77.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mkuu anaeleza kuwa katika nia ya kutaka kutoa mafunzo ya ufundi stadi sambamba na mahitaji ya soko la ajira, VETA iliendelea kufanya utafiti wa soko la ajira katika maeneo mbalimbali.
“Tumefanikiwa kufanya utafiti wa soko la ajira katika maeneo 7 kwenye sekta za Ufundi Magari, Mavazi na Nguo, Kilimo na Usindikaji wa Chakula, Uchapaji, Nywele na Urembo, Umeme na Uziduzi (Uchimbaji na Uchakataji Madini). Sambamba na hilo, mitaala 19 ama iliandaliwa au kufanyiwa mapitio kulingana na taarifa za mahitaji ya soko la ajira,” anasema.
Eneo lingine muhimu lililoendelea kutekelezwa na Mamlaka na kupata msaada wa Serikali ya Awamu ya Sita ni uendelezaji ubunifu katika eneo la ufundi stadi. Miongoni mwa mafanikio katika eneo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni pamoja na kutambua jumla ya wabunifu 117 wakiwa ni kutoka Vyuo vya Ufundi Stadi na Mfumo Usio Rasmi katika zoezi la Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU). Wabunifu Kumi Bora katika kila kundi walishiriki Fainali za MAKISATU zilizofanyika Jijini Dodoma, tarehe 6 hadi 11 Mei, 2021.
Sambamba na hilo, VETA imewezesha wabunifu kushiriki katika Maonesho mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa. Ubunifu wa walimu na wanafunzi wa VETA ulikuwa kivutio kikubwa kwa watu waliotembelea maonesho na ulichangia kupata ushindi. Mathalani, katika Maonesho ya Sabasaba, VETA iliibuka Mshindi wa Kwanza kwenye Kundi la Uendelezaji Ujuzi na kwenye Maonesho ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania ilikuwa miongoni mwa Mabanda Bora.
“Tumeendelea pia kujenga na kuimarisha ushirikiano na Makampuni na Taasisi mbalimbali zenye malengo na mwelekeo unaofanana na shughuli zetu ili kuimarisha utoaji mafunzo, kusaidia vijana kupata mafunzo bora na fursa za ajira, pamoja na kuchangia katika kuisaidia serikali kupata rasilimali kwa ajili ya uendelezaji ujuzi,” Mkurugenzi Mkuu anasema.
Anataja miongoni mwa ushirikiano kuwa ni wa Chemba ya Wachimbaji Madini (TCM) katika kutekeleza Mradi wa IMTT; Shirika la Kimataifa la Care katika utoaji mafunzo ya Kilimo na Ufugaji kupitia Mradi wa Tajirika na Kilimo; taasisi ya WHKT ya Ujerumani katika kuendeleza na kueneza mafunzo ya Ufundi wa Zana za Kilimo (Agro-mechanics) katika vyuo vya VETA vya Arusha, Kihonda, Mpanda na Dakawa; Mashirika la ECLAT Development Foundation na UPENDO kuendeleza Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Simanjiro; na Ushirikiano na Benki ya KCB, kupitia programu yake ya 2Jiajiri, kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana 200 katika Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Dar es Salaam.
Kusaidia makundi maalum kupata fursa za mafunzo ya ufundi stadi pia limekuwa eneo la kuzingatiwa. Kwa kushirikiana na wadau, VETA iliendelea kuweka mipango na kufanya juhudi mbalimbali ili kukuza fursa za upatikanaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa makundi yote. Juhudi hizo zimewezesha kudahili vijana 663 wenye ulemavu kwenye kozi za muda mrefu na wengine 998 wenye changamoto mbalimbali za kiuchumi (sawa na asilimia 166 ya lengo la mwaka). Udahili wa wanafunzi wa kike nao uliongezeka kutoka asilimia 37 hadi asilimia 41.
Mkurugenzi Mkuu anaishukuru serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele kikubwa elimu na mafunzo ya ufundi stadi na kusema kuwa VETA itaendelea kutekeleza maagizo ya serikali kwa uzito mkubwa huku ikiweka mipango na juhudi thabiti kupanua fursa za elimu na mafunzo hayo kwa manufaa ya nchi na wananchi wake.