Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetenga Sh. bilioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo 25 vya Ufundi Stadi katika Wilaya mbalimbali nchini.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Urambo tarehe 9 Julai 2019, Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema ujenzi wa vyuo hivyo ni utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata fursa za mafunzo ya Ufundi Stadi.
Prof. Ndalichako amesema vyuo hivyo vinatarajiwa kujengwa katika Wilaya za Chunya, Kilindi, Korogwe, Ukerewe, Igunga, Pangani, Kishapu, Rufiji, Uyui, Kwimba, Bahi, Mafia, Longido, Mkinga, Uvinza, Ikungi, Iringa vijijini, Lushoto, Mbarali, Monduli, Buhigwe, Ulanga, Masasi, Butiama na Chemba.
Amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha inakuwa na chuo cha Ufundi Stadi katika kila Wilaya na Mkoa ili kuendana na kasi na maono ya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda.
“Hatuwezi kuzungumzia uchumi wa viwanda bila kuwa na watu wenye ujuzi ambao ndio wataenda kufanya kazi katika viwanda ndiyo maana Wizara yangu imeongeza kasi ya ujenzi wa vyuo vya VETA nchini,” Alisema
Waziri Ndalichako amesema kuwa kwa sasa Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa vyuo vya Wilaya za Nkasi, Ileje, Newala, Muleba, Kasulu, Itilima, Ngorongoro, Chato na Babati vinavyotarajiwa kumalizika ndani ya mwaka 2019 na matayarisho yanaendelea ya kuanza ujenzi wa vyuo vya Ufundi stadi katika Wilaya za Kongwa, Ruangwa, Nyasa na Halmashauri ya mji wa Kasulu.
Kwa ngazi ya Mkoa, Prof. Ndalichako amesema kuwa ujenzi wa vyuo vya Mikoa ya Geita na Rukwa unaendelea na kwamba ujenzi wa vyuo vya Mikoa ya Simiyu, Ludewa na Kagera utaanza punde.
Alisema kuwa serikali inaamini kuwa chuo hicho cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Urambo kitakuwa chachu ya maendeleo ya viwanda Mkoani Tabora na kuwataka wananchi wakitumie vyema katika kujipatia ujuzi.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri alisema kuwa chuo cha VETA Urambo kimekuja wakati mwafaka ambapo changamoto ya ukosefu wa ujuzi ni kubwa hali inayosababisha vijana kukosa ajira kwenye miradi mbalimbali mkoani hapo.
Aliwasisitiza wananchi wa Urambo kutumia vyema chuo hicho kupata ujuzi wa aina mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji halisi ya soko la ajira ili waweze kujiajiri.
“Tufike mahali vijana wetu wa mkoa wa Tabora wakiulizwa unataka kuwa nani waseme wanataka kuwa waajiri wa watu wengine”Alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Peter Maduki alisema kuwa VETA imedhamiria kuongeza udahili wa mafunzo ya Ufundi stadi nchi nzima, kuboresha ufundishaji kwa kuongeza vifaa na walimu pamoja na kuboresha miundombinu.
Alisema kuwa VETA imejipanga kukuza uzalishaji katika viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kwa kufanya ubunifu utakaowezesha kuanzishwa kwa viwanda pamoja na kurahisisha uchakataji wa mazao mbalimbali.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu alisema kuwa chuo cha Urambo kilitokana na kukarabatiwa kwa majengo yaliyotumiwa na mkandarasi aliyejenga barabara ya Ndono hadi Urambo na kisha kukabidhiwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo na baadae Halmashauri hiyo kuyatoa yatumike kunzisha chuo hicho kutokana na uhitaji mkubwa wa Chuo cha Ufundi Stadi katika Wilaya hiyo.
Alisema jumla ya kiasi cha Sh. milioni 218 zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa chuo hicho chenye majengo 15 yatakayotumika kwa ajili ya madarasa, karakana, ofisi, mabweni na nyumba za walimu.
Dkt Bujulu alizitaja fani zitakazotolewa katika chuo hicho kwa kuanzia kuwa ni Umeme wa Majumbani, Ushonaji, Ujenzi, na Uhazili na matumizi ya Kompyuta na kina uwezo wa kudahili wanafunzi 160 kwa mafunzo ya muda mrefu na wanafunzi zaidi ya wanafunzi 500 wa kozi za muda mfupi kwa mwaka.
Aliiomba Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kuwaongezea eneo zaidi linalopakana na chuo hicho kwa ajili ya kuongeza madarasa, karakana na mabweni ili kuongeza udahili wa wanafunzi kwa kuongeza fani mbalimbali kama vile fani za kilimo na ufugaji, Uungaji na Uundaji vyuma, ufundi mekanika, ufundi bomba, n.k. kwa kadri ya mahitaji ya soko.
Naye Mbunge wa Urambo Mashariki Magareth Sitta aliipongeza VETA kwa kufanikisha ukarabati wa chuo hicho na kuwataka wazazi kuwapeleka watoto katika chuo hicho wajipatie ujuzi. Ili kuleta hamasa kwa wazazi kuleta watoto wao katika chuo hicho, Mbunge huyo aliahidi kuwalipia ada ya kiasi cha Sh. 60,000 kwa kila mwanafunzi kwa wanafunzi 62 kutoka katika viijiji mbalimbali Wilayani hapo.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office