Hatua nyingine imehesabika katika jitihada za kusogeza huduma za mafunzo ya ufundi stadi kwa wananchi baada ya chuo cha ufundi stadi cha wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara kuzinduliwa.
Uzinduzi wa chuo hicho kilichopo katika kijiji cha Emboreet, Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro umefanywa Jumamosi ya tarehe 19 Oktoba 2019 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako katika tukio ambalo lilihudhuriwa pia na viongozi wa ngazi ya juu wa wilaya na halmashauri ya Simanjiro na wananchi wa wilaya hiyo kwa ujumla.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Peter Maduki, Prof. Ndalichako alisema serikali inatambua umuhimu mkubwa wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi katika maendeleo ya nchi, hasa katika kipindi hiki cha mwelekeo wa serikali kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.
Alisema, serikali inaendelea kujenga vyuo vya ufundi stadi na inatarajia kuwa kabla ya mwisho wa mwaka huu vyuo vinavyomilikiwa na serikali kupitia VETA vitafikia 40, jambo ambalo litasaidia zaidi kusogeza huduma za mafunzo ya ufundi stadi karibu na wananchi.
“Kwa taarifa nilizonazo ni kuwa vyuo vya VETA vya Wilaya za Nkasi, Ileje, Muleba na Itilima vimekamilika na viko tayari kwa uzinduzi, hivyo tutavizindua muda wowote kabla ya mwisho wa mwezi Novemba mwaka huu. Pia vyuo vya VETA vya Halmashauri za Kilindi, Ngorongoro, Babati na Newala viko katika hatua za mwisho za ukamilishwaji, hivyo vitazinduliwa kabla ya mwisho wa mwaka huu,” alisema.
Aliongeza kuwa ujenzi wa vyuo vya mikoa unaendelea katika mikoa ya Rukwa na Geita na mchakato wa kuanza ujenzi wa vyuo vya wilaya za Kongwa, Kasulu T.C., Nyasa na Ruangwa uko katika hatua za mwisho, lengo likiwa ni kuanza ujenzi kabla ya mwisho wa mwezi Oktoba 2019.
Aliipongeza VETA kwa juhudi hizo kubwa za kuongeza wigo wa kuzalisha rasilimali watu yenye ujuzi mahsusi kwa ajili ya kukuza uchumi wa Taifa na maendeleo kwa ujumla.
Maduki alitumia fursa hiyo pia kuuomba uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kuwatumia vijana watakaohitimu fani ya Uashi katika chuo cha VETA Simanjiro pale wanapokuwa na miradi ya ujenzi kwa njia ya Force Account ili vijana hao waweze kunufaika na ajira kwenye eneo lao na kuchangia katika ujenzi wa wilaya yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu aliyashukuru mashirika ya ECLAT Development Foundation la Wilayani Simanjiro na Upendo la Ujerumani pamoja na wananchi wa Wilaya ya Simanjiro kwa ujumla kwa kushiriki kwa kiasi kikubwa katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho.
Alisema juhudi zao zimeonesha mfano hai wa kuunga mkono kwa vitendo juhudi za kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa Watanzania.
“Wamefanya jitihada kubwa katika ujenzi wa chuo hiki kwa awamu ya kwanza ambao umehusisha madarasa matano; bweni moja la kulaza wanafunzi wa kike 48; nyumba ya Mwangalizi (Matron); jiko moja; matundu 32 ya vyoo; kisima kirefu cha maji; pampu ya maji inayoendeshwa na nguvu ya jua; matenki ya kuhifadhia maji; uzio wa seng’enge kuzunguka chuo; mfumo wa umeme wa jua; pamoja na samani na vifaa vya kufundishia na kujifunzia,” alisema.
Alisema, ili kuchangia juhudi hizo, kuongeza udahili na kukiimarisha zaidi chuo hicho, VETA imeamua kujenga bweni la wavulana lenye uwezo wa kulaza vijana 48 na nyumba ya Patron sawasawa na lile lililojengwa kwa ajili ya wanafunzi wa kike ili kuleta uwiano sawia wa kijinsia.
“Ujenzi huu tunaufanya kwa fedha za serikali, (bajeti ya VETA) kwa kutumia wataalam na mafundi wetu wa ndani, yaani Force Account na utagharimu kiasi cha Sh. milioni 82 ikiwa ni pamoja na mifumo ya umeme na maji na ununuzi wa vitanda, magodoro na makabati ya vyumbani. Tunatarajia kuukamilisha kabla ya mwisho wa mwaka huu wa 2019. Tutaendelea kuweka mipango na bajeti kwa kadri ya uwezo wetu ili kukiimarisha zaidi chuo hiki ili kiwanufaishe wananchi, hususani vijana wa wilaya hii ya Simanjiro,” alifafanua.
Alisema tayari chuo hicho kimeshaanza kutoa mafunzo ambapo vijana 24 wamedahiliwa katika fani ya Uashi tangu tarehe 31 Julai 2019, kati yao watatu ni wa kike.
Aliongeza kuwa VETA imejipanga kuendelea na udahili mwezi Januari 2020 ambapo wanafunzi wengine 20 katika fani ya Uashi na 20 fani ya umeme watadahiliwa na wote kupatiwa malazi katika mabweni ya chuoni hapo.
Naye Mwenyekiti wa Shirika la Upendo la Ujerumani, Dkt. Fred Heimbach aliishauri VETA kutoa kipaumbele kwa vijana wa Simanjiro inapofanya udahili wa wanafunzi kwa ajili ya mafunzo katika chuo hicho, kwani kwa uchunguzi wake amebaini kuwa vijana wengi wilayani humo wana uhitaji mkubwa wa mafunzo ya ufundi stadi.
Hafla hiyo pia iliambatana na kubadilishana rasmi nyaraka za makabidhiano ya umiliki wa chuo hicho kati ya Shirika la ECLAT la Wilayani Simanjiro, Upendo la Ujerumani na VETA.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office