The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, amewaasa watumishi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuzingatia utunzaji wa afya zao, kwani ndio mtaji katika kazi zao.
CPA Kasore ametoa wito huo, Ijumaa, tarehe 29 Septemba 2023, wakati akifungua semina kuhusu UKIMWI na magonjwa yasiyoambukizwa kwa wafanyakazi wa VETA Makao Makuu, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Dodoma.
“Usije ukafikiri barua yako ya ajira ndio mtaji, afya yako ndio mtaji. Afya yako ikitetereka kazi inaweza isifanyike. Kwa hiyo tunza afya yako,” Amesema.
Amesema Serikali inawekeza nguvu nyingi kwa watumishi wake, hivyo nao wanapaswa kutunza vyema afya zao ili waweze kuitumikia vyema.
Amewaasa watumishi kuzingatia elimu inayotolewa na madaktari na wataalamu wa afya ambao wamekuwa wakialikwa na VETA kuja kutoa mafunzo kwa watumishi wake.
Pia amewakumbusha kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara, ikiwa ni miongoni mwa njia muhimu ya kudhibiti magonjwa yasiyoambukizwa.
Semina hiyo ilihusisha elimu ya UKIMWI na magonjwa yasiyoambukizwa yakiwemo Magonjwa ya Akili, Kisukari na Shinikizo la Damu.