The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
UJUMBE KUTOKA ETHIOPIA WATEMBELEA VETA KUJIFUNZA PROGRAMU YA URASIMISHAJI UJUZI
Posted on: Tuesday, 12 March 2024
UJUMBE KUTOKA ETHIOPIA WATEMBELEA VETA KUJIFUNZA PROGRAMU YA URASIMISHAJI UJUZI
Ujumbe wa wataalamu kutoka Wizara ya Kazi na Ujuzi ya nchini Ethiopia wametembelea Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kujifunza juu ya utekelezaji wa programu ya Urasimishaji Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo (Recognition of Prior Learning-RPL).
Wakiwa katika ofisi za VETA Makao Makuu, jijini Dodoma, leo, tarehe 11 Machi, 2024, wajumbe hao walipokea maelezo kuhusu utekelezaji wa programu hiyo hapa nchini, ,manufaa yaliyopatikana na changamoto zake, tangu VETA ilipoanza kutekeleza programu hiyo kwa majaribio mwaka 2009.
Kaimu Mkurugenzi wa Utahini na Utunuku, Francis Komba, amesema tangu kuanzishwa kwa programu hiyo, jumla ya wanagenzi 23,460 wamerasimishiwa ujuzi wao na kutunukiwa vyeti.
Amesema Serikali ya Ethiopia imeamua kutuma wataalamu hao nchini Tanzania kujifunza juu ya programu hiyo ili kuwezesha nchi hiyo kuanzisha programu hiyo na kwamba Tanzania imetambuliwa kuwa nchi inayofanya vizuri zaidi kwenye uendeshaji wa programu ya RPL.
Nchi ya Malawi ni miongoni mwa nchi zilizofanikiwa kuanzisha na kutekeleza programu ya RPL baada ya kutembelea Tanzania na kujifunza juu ya programu hiyo mwaka 2022.
RPL ni mchakato wa kutambua, kutathmini na kuthibitisha ujuzi wa mtu bila kujali namna alivyoupata ujuzi, lini, wapi na kwa muda gani ujifunzaji umefanyika.
Kupitia mpango huu, mhusika (mwanagenzi) hufanyiwa tathmini ya ujuzi wake ili kutambua umahiri alionao, mapungufu yake na hatimaye VETA kumpatia mafunzo kisha kumtathmini na hatimaye kutunuku cheti kwa aliyefaulu tathmini hiyo.
Katika ziara hiyo, wataalamu hao watapata fursa ya kuwatembelea wanagenzi wanufaika wa programu hiyo waliopo jijini Dodoma.