The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Uzinduzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Mkoa wa Kagera - Kielelezo cha kuenzi fikra za Baba wa Taifa
Posted on: Wednesday, 09 November 2022
Mwaka huu mkoa wa Kagera ulikuwa mwenyeji wa Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru na Kumbukizi ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambayo hufanyika tarehe 14 Oktoba ya kila mwaka. Vilevile, mkoa huo ulikuwa mwenyeji wa Wiki ya Vijana ambayo hufanyika tarehe 8 hadi 14 Oktoba ya kila mwaka. Maadhimisho ya Wiki ya Vijana, Kumbukizi ya Hayati Mwalimu Nyerere na Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru vimeambatana na zawadi ya kipekee kwa wana Kagera na Watanzania kwa ujumla. Zawadi hiyo ni makabidhiano na uzinduzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera.
Makabidhiano na uzinduzi wa chuo hicho ulifanyika tarehe 13 Oktoba mwaka huu, Mgeni Rais akiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera (Kagera RVTSC) kimejengwa kwa hisani ya Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Mradi wa ujenzi wa chuo hicho umetekelezwa katika eneo la Muhengere, kijiji cha Burugo, kata ya Nyakato, Wilaya ya Bukoba vijijini Mkoa wa Kagera. Mradi wa ujenzi wa chuo hicho umegharimu jumla ya dola za Kimarekani 9,552,380 sawa na fedha za kitanzania shilingi Bilioni 22. Fedha hizo zinajumuisha shughuli za ujenzi, usimamizi na uwekwaji wa baadhi ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia, mashine na samani katika majengo. Makubaliano ya utekelezaji wa mradi yalikuwa ni miezi 18 kuanzia tarehe 28 Novemba 2019 hadi tarehe 27 Mei 2021. Hata hivyo, kutokana na changamoto mbalimbali, Mkandarasi aliomba kuongezewa muda na kuruhusiwa kukamilisha mradi tarehe 30 Aprili 2022.
Utekelezaji wa mradi huu umehusisha majengo na miundombinu ikiwemo majengo matatu ya karakana za mafunzo; jengo la Madarasa, ukumbi wa mihadhara, maabara ya kompyuta na chumba cha maktaba; jengo la ofisi za walimu na jengo la Utawala linalojumuisha maofisi mbalimbali. Majengo mengine ni nyumba mbili za walimu zenye kuchukua familia nne; mabweni mawili ya Wanafunzi; jengo la jiko na bwalo la chakula; jengo la Mitambo na mifumo ya kusambaza umeme na maji;ghala (store) na jengo la walinzi na lango kuu la kuingilia. Pia ulihusisha miundombinu wezeshi ikiwa ni pamoja na uzio, usawazishaji ardhi kwa ajili ya viwanja vya michezo; barabara za ndani, maeneo ya maegesho, mataa ya barabarani na mitaro ya kusafirisha maji ya mvua. Pia mifumo ya vyoo na mifumo ya ukusanyaji maji taka; mifumo ya kupambana na majanga ya moto; mifumo ya CCTV kamera, Internet, TV na sauti; ununuzi wa Transformer 1 yenye 315kVA na uwekwaji wa baadhi ya mashine, mitambo na zana mbalimbali za kufundishia na kujifunzia pamoja na samani.
Akizungumzia uwezo wa chuo hicho, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, alisema chuo kitakuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 400 wa kozi za muda mrefu na Wanafunzi 1,000 wa kozi za muda mfupi. Pia Chuo kitaweza kutoa Huduma ya malazi kwa wanafunzi 320 ikiwa wa kike 104 na wa kiume 216.
“Mradi huu umekuwa na faida kwa kipindi chake cha utekelezaji kwani umeweza kuwapatia ajira vijana na watoa huduma mbalimbali zaidi ya 300 kwenye maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa mradi. Aidha, ujenzi wa chuo hiki unaenda kuwezesha ufanyikaji wa shughuli za kiuchumi katika maeneo yanayozunguka chuo hiki,” aliongeza.
Kukamilika kwa chuo hiki kuna tafsiri gani katika harakati za kupanua fursa za elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini? Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia alifafanua kuwa kukamilika kwa Chuo hicho kutawezesha kuongeza fursa za elimu ujuzi kwa vijana nchini hasa vijana wa mkoa wa Kagera na kuwawezesha kujipatia ajira.
“Mheshimiwa Rais umekuwa ukisisitiza sana mambo mawili katika elimu… kwanza ubora wa elimu na pili elimu yenyewe itoe ujuzi wa kumwezesha mhitimu kumudu mazingira anayoishi na utandawazi…. utakumbuka Mheshimiwa Rais ulituagiza kukamilisha ujenzi wa vyuo vya VETA katika mikoa yote ambayo haina vyuo vya ngazi ya mkoa…leo hii Mheshimiwa Rais unapokea hiki chuo ambacho sasa kinaiweka Kagera kati ya mikoa ambayo tayari ina vyuo vya VETA vya mikoa,” alisema.
Ilifika wakati muhimu wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuzungumza na wananchi. Hotuba ya Mheshimiwa Rais ilijaa uchambuzi mpana juu ya umuhimu wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi na namna ya kutumia vyema fursa hizo. Alifafanua pia juu ya juhudi ambazo zinafanywa na serikali yake na wadau wa maendeleo katika kupanua fursa za elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Alisema umuhimu mkubwa wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi ni kuwezesha watu kupata stadi za kutenda kazi halisi katika fani zao na kwamba unaenda sambamba mahitaji ya nguvukazi katika ulimwengu wa sasa. Vilevile, tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana, ufundi stadi ni eneo la msingi kabisa katika kuchangia kupunguza tatizo hilo, kwani unampa mtu fursa ya kuajiriwa kwa ujira au kujiajiri mwenyewe.
“Tunazungumzia tatizo la kutokuwa na ajira, tunasomesha watoto lakini hawana ajira… Kazi yetu ni kuhakikisha asilimia hii 12 tunaijengea uwezo ,tunaipa ujuzi ili iweze kujiajiri na kuajiriwa,” alisema.
Alisema, mafundi stadi wengi wanahitajika pia katika utekelezaji wa Miradi ya Kimkakati tuliyonayo kama Mradi wa Umeme wa Mwalimu J. K. Nyerere Hydro-power; Reli ya Kisasa-SGR; Bomba la Mafuta kutoka Tanzania mpaka Uganda, usambazaji umeme kupitia REA, pamoja na ujenzi wa shule na vituo vya afya katika halmashauri mbalimbali nchini.
Wananchi wanazungumziaje ujenzi na fursa zinazotarajiwa baada ya chuo hiki kuzinduliwa?
“Uwepo wa chuo hiki ni fursa kwa wakazi au majirani ambao ni kijiji cha Burugo lakini pia na wakazi wa mkoa wa Kagera ambao pia wanaweza kutumia chuo hiki kwa vijana wao kujisomea au kupata fani mbalimbali lakini pia kujipatia ajira,” Hemedi Musa, Mkazi wa kijiji cha Burugo.
Diwani wa kata ya Nyakato, Mhe. Laurent Rwezimura, amewataka wananchi wa kata hiyo kushirikiana kwa karibu na uongozi wa chuo hicho kulinda miundombinu ya chuo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kunufaisha vijana wengi Zaidi.
Uzinduzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera umeakisi madhumuni ya kuwashwa na kukimbizwa kwa Mwenge wa Uhuru, umeleta tumaini jipya kwa wana Kagera; umeakisi fikra za Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere juu ya Elimu ya Kujitegemea na umeyatafsiri vyema maadhimisho ya Wiki ya Vijana kwa kuwakumbusha juu ya umuhimu wa ujuzi katika kujiletea maendeleo yao na ya nchi kwa ujumla. Kilichobaki kwa wana Kagera sasa ni kuhamasishana kutumia fursa ya uwepo wa chuo hiki katika kupata ujuzi na kujiletea maendeleo.