The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VET Board yashauriana na watendaji wa VETA juu ya kuimarisha, kuboresha huduma
Posted on: Wednesday, 07 August 2024
Bodi ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VET Board), jana, tarehe 6 Agosti, 2024, imefanya kikao cha mashauriano na Menejimenti na watendaji wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kuhusu maendeleo ya utoaji mafunzo, huduma na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali ili kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Chuo cha VETA Dodoma, jijini Dodoma na kuwahusisha Mwenyekiti na wajumbe wa Bodi, Menejimenti ya VETA Makao Makuu na Wakurugenzi wa Kanda.
Katika kikao hicho, Mwenyekiti wa VET Board, Prof. Sifuni Mchome, alisema kuwa Bodi imependekeza kikao hicho ili kuwezesha kupata mawazo mengi na kupata fursa pana ya mashauriano zaidi badala ya Bodi kuendelea kupokea kilichotekelezwa au kilichopangwa na kutoa maelekezo.
“Kuna mambo mengi ya kimkakati tunatakiwa kuyafanyia kazi. Mathalani, uwiano wa mafundi stadi, mafundi sanifu na wahandisi si nzuri sana hapa nchini. Tunatakiwa kujipanga kurekebisha hizo dosari,” amesema Prof. Mchome.
Ameongeza kuwa, wananchi katika maeneo mbalimbali wana changamoto nyingi ambazo ukitazama VETA inaweza kuwa na ufumbuzi wake.
“Tanga wanavuna matunda mengi sana, lakini takribani nusu yanaharibika. Wananchi wa Dodoma wanalima zabibu, lakini si nyingi sana kwa sababu ni kilimo kinachohitaji nguvukazi na gharama kubwa. VETA inaweza kubuni teknolojia kuwasaidia wakulima hao,” amefafanua.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru, akiwa miongoni mwa wageni walioalikwa kuchokoza mada ameishauri VETA kuwa na mtazamo wa kimataifa kwa kuangalia fursa mbalimbali zilizopo.
Sambamba na hilo Mafuru akaishauri jamii kuondokana na mtazamo kuwa VETA ni mahala pa walioshindwa, bali ni mahala pa kunoa watu wenye vipaji na wale wanaofanya bidi ya kujikwamua.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi zisizo za Kibiashara, kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Dkt. Emmanuel Luvanda amewashauri viongozi na watendaji wa VETA kubuni mbinu mbalimbali za kupata rasilimali kwa ajili ya kusaidia kuendesha mafunzo na shughuli zingine za Mamlaka.
Amesema, zipo fursa nyingi za kuwezesha kupata rasilimali, ikiwemo kuanzisha kampuni na kuandika maandiko mbalimbali kuomba fedha na msaada wa vifaa kama magari na mashine ambazo ziko katika mpango wa kupigwa mnada baada ya kutumika kwenye taasisi za Serikali na Sekta Binafsi.
Kikao hicho cha mashauriana kilialika wachokoza mada kutoka Tume ya Mipango nchini, Ofisi ya Msajili wa Hazina na timu ya wataalam waliofanya tathmini ya Mpango Mkakati wa VETA, wakiongozwa na Prof. Simon Msanjila kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma.