Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeingia makubaliano na Shirika la Kimataifa la Care na Asasi ya Ukuzaji Kilimo Uwanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) kutekeleza mradi unaolenga kujenga na kuimarisha ujuzi katika sekta ya kilimo, hususani kwa makundi maalum katika mikoa ya Iringa, Njombe na Morogoro.
Makubaliano ya mradi huo uliopewa jina la Tajirika yalisainiwa jana, 28 Novemba 2018 katika ofisi za VETA Makao Makuu na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt Pancras Bujulu, Afisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT, Goeffrey Kirenga na Naibu Mkurugenzi wa Sera na Programu wa Care nchini Tanzania , Gloria Cheche.
Mradi huo unatarajiwa kuwanufaisha 2200 kutoka makundi maalum, ambapo kati yao 70% ni wa kike kwa kuwapatia msaada wa kifedha na vifaa vya mafunzo ili waweze kuhudhuria na kujifunza ufundi stadi.
Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu alisema ushirikiano huo unalenga kuimarisha ubora wa mafunzo ya ufundi stadi na kuendeleza ujasiriamali katika eneo la kilimo kwa jamii za watu waishio vijijini nchini Tanzania.
“Tumebaini hitaji kubwa la ujuzi wa ufundi stadi kwenye sekta ya kilimo, maana kuna vijana wengi wamekuwa wakijishughulisha na kilimo bila ya kuwa na ujuzi maarifa sahihi. Kwa hivyo kunakuwa hakuna ufanisi na tija inakuwa ndogo,” alisema.
Alisema Mamlaka sasa inaweka mipango na mikakati mbalimbali kuimarisha mafunzo katika eneo la kilimo na ushirikiano na wadau hao wawili unachangia kwenye juhudi za Mamlaka kutoa mafunzo yanayogusa kilimo. Katika kutekeleza mradi huo, VETA itaandaa mitaala, kufundisha walimu wa walimu, kutoa mafunzo yenye lengo la kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchangia taarifa za mahitaji ya soko katika kilimo.
Naibu Mkurugenzi wa Sera na Programu wa Care nchini Tanzania , Gloria Cheche alisema shirika lake lilivutiwa kushirikiana na VETA kwa kutambua kuwa kupitia VETA ni rahisi kuwapata vijana wengi nchini.
“tunatambua pia kuwa kwa kufanya kazi na VETA ni rahisi pia kuwafikia watu wa makundi maalum katika jamii na kuwawezesha kujikwamua kimaisha kwa kuwafundisha ujuzi wa kuajirika,” alisema.
Alisema Care International ambayo itakuwa ndio msimamizi na mratibu mkuu wa mradi, pamoja na mambo mengine, itawashirikisha wadau wote na kujenga mahusiano mazuri na serikali kuu na serikali za mtaa katika kutekeleza mradi katika maeneo husika.
Afisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT Goeffrey Kirenga alishukuru kuanza kwa ushirikiano huo akisema kuwa kilimo kinaendelea kupanuka sambamba na mahitaji ya ujuzi katika sekta hilo.
Alisema ushirikiano ulioanzishwa utasaidi kushughulikia changamoto za mahitaji ya ujuzi, hasa kwenye maeneo ya usindikaji na uhifadhi wa mazao ya kilimo.
Katika mradi huo ambao mafunzo yatatolewa zaidi kwenye jamii, SAGCOT itachangia katika kutoa taarifa za mahitaji ya soko la ajira kwenye eneo la kilimo, hasa mtazamo wa sekta binafsi pamoja na vipaumbele vinavyoweza kuingizwa kwenye mitaala ili wahitimu waweze kuajirika kwa urahisi.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office