Kwa kuzingatia mahitaji ya ujuzi kwenye sekta za Kilimo na Mifugo, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) iko katika hatua za juu za majadiliano na Chuo cha Ufundi Stadi wa Kilimo Henan cha nchini China kwa lengo la kuanzisha chuo maalum cha ufundi stadi kitakachobobea katika utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi katika fani za Kilimo na Mifugo.
Ujumbe wa timu ya viongozi na wataalam 9 kutoka Chuo cha Henan, ukiongozwa na Makamu wa Rais wa Chuo hicho, Prof. Wu Guozhao, umekuwepo nchini kwa siku mbili, tarehe 18 na 19 Desemba 2019 kwa ajili ya kutembelea vyuo vya VETA na kufanya mazungumzo ya awali na Menejimenti ya VETA juu ya mpango huo. Timu hiyo ilitembelea na kujionea mazingira na hali halisi ya utoaji mafunzo katika vyuo vya VETA Kihonda kinachotoa mafunzo katika Fani ya Ufundi wa Zana za Kilimo na Chuo cha TEHAMA cha VETA Kipawa. Ikiwa Morogoro, timu hiyo ilipata pia fursa ya kutembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa lengo la kupanua zaidi ufahamu wa mafunzo ya kilimo yanavyotolewa nchini.
Akizungumzia wakati wa majadiliano na ujumbe huo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu amesema ana imani kubwa kuwa mpango wa ujenzi wa chuo hicho utawavutia wengi na unagusa sekta ya kipaumbele kikubwa katika jamii.
Alisema asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi kwa kutegemea kilimo na hata wafanyakazi na wafanyabiashara wengi nchini pia wanapenda kujishughulisha na kilimo.
“Mathalani, kwa miaka mingi watu wengi wanaulizia mafunzo ya Kilimo cha Mazao ya Bustani, Usindikaji wa Mazao ya Chakula na hata Kilimo cha Mazao ya Nafaka. Kwa ujumla naona kuna mahitaji mengi ya ujuzi katika eneo la kilimo. Bila shaka mpango huu utaungwa mkono na Serikali yetu tukufu ya awamu ya tano,” alisema Dkt. Bujulu.
Alisema VETA ina nia ya kuimarisha mafunzo katika sekta ya Kilimo na Mifugo na miongoni mwa malengo ni kuwa na chuo mahsusi kitakachobobea na kuwa kituo bora cha mfano katika mafunzo ya ufundi stadi kwenye sekta za Kilimo na Mifugo.
Katika vyuo vinavyomilikiwa na VETA, mafunzo ya muda mrefu ya ufundi stadi yanayogusa sekta ya kilimo hutolewa katika fani za Ufundi wa Zana za Kilimo (VETA Kihonda, VETA Manyara, VETA Arusha-Oljoro, VETA Mpanda na VETA Dakawa); Ufugaji (VETA Singida); Teknolojia ya Usindikaji wa Nyama (VETA Dodoma). Vilevile VETA huendesha kozi za muda mfupi ambazo ni za kati ya miezi miwili hadi sita kupitia programu yake ya Uboreshaji Ujuzi kwa Wajasiriamali kwenye Sekta Isiyo Rasmi (INTEP) ukihusisha mafunzo mbaimbali kama Kilimo cha Uyoga, Ufugaji wa Samaki, Utengenezaji Mvinyo, Usindikaji wa Mboga na Matunda, Usindikaji wa Samaki na Usindikaji wa Asali.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Chuo cha Henan, Wu Guozhao amesema ni vyema kuweka mpango maalum wa utekelezaji wa wazo hilo la kujenga chuo kwa ushirikiano na kuhakikisha kuwa pande mbili zinauridhia kabla ya kuanza kuutekeleza hatua kwa hatua.
“Hata sisi tunahitaji ridhaa ya Serikali yetu. Chuo chetu kinaendeshwa kwa fedha za serikali, tunaweza kupata msaada wa serikali kwa kiwango fulani. VETA nanyi mnapaswa kuzungumza na serikali ili kupata ridhaa yake na kuomba ufadhili kwa ajili ya ujenzi na uendeshaji wa chuo hicho,” amesema Guozhao.
Ameongeza chuo cha Henan kitatumia uzoefu wake katika mafunzo mbalimbali kwenye eneo la Kilimo na kushirikiana na VETA katika kubuni na kuanzisha kozi ambazo zitawiana na mahitaji ya Watanzania.
Mazungumzo hayo yamehitimishwa kwa makubaliano ya VETA kuandaa Andiko la Mradi wa Chuo cha Ufundi Stadi wa Kilimo na kuainisha na kuliwasilisha kwa Serikali ya Tanzania ili kupata ridhaa yake, kabla ya hatua zingine za majadiliano ya utekelezaji kuendelea.
Miongoni mwa mambo ambayo Andiko hilo linapaswa kuainisha ni muundo utekelezaji wa majukumu na ushiriki wa pande zote mbili (yaani Chuo cha Henan na VETA) katika gharama za ujenzi; ununuzi wa vifaa; uandaaji wa mitaala; muundo wa fani; utungaji mitihani na utoaji vyeti na usimamizi wa chuo. Vilevile, imekubalika kuwa Andiko linatakiwa kupendekeza mahali pa kujenga chuo kwa kuzingatia vigezo mbalimbali pamoja na kuainisha kozi zitakazofundishwa na utaratibu wa kuanza kwa kozi hizo hatua kwa hatua. Tayari VETA na Henan zilishasaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) katika maeneo mbalimbali ya utoaji mafunzo na uendelezaji ujuzi tangu Desemba mwaka jana na hatua mbalimbali za utekelezaji wa MoU hiyo zimeshafanyika ikiwa ni pamoja na kutembeleana na kubadilishana uzoefu. Miongoni mwa matunda ya hivi karibuni ya makubaliano ufadhili na Chuo cha Henan kwa walimu 10 kutoka vyuo mbalimbali vya ufundi stadi kujiunga na mafunzo ya miaka mitatu katika fani mbalimbali za kilimo katika chuo hicho nchini China. Walimu hao wataondoka mapema Februari 2020 kwa ajili ya kwenda kuanza masomo. Chuo cha Henan cha Ufundi Stadi wa Kilimo (Henan Vocational College of Agriculture) kilianzishwa mwaka 1952. Chuo hicho kilichopo katika jimbo la Henan kinachomilikiwa na serikali ya China ni chuo cha mfano katika utoaji wa elimu ya ufundi stadi katika fani mbalimbali za kilimo ikiwa ni pamoja na kilimo cha bustani na mbogamboga, ufugaji na usindikaji wa chakula.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office