The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Mwitikio wa watu wengi kwenye mabanda ya VETA wakati wa maonesho unaashiria namna ambavyo Watanzania wanazidi kutambua thamani ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi. Katika maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (Sabasaba) na ya kilimo (Nanenane), kumekuwa na wananchi wengi wakifurika katika mabanda ya VETA ili kupata taarifa za mafunzo na kujionea ubunifu wa aina mbalimbali uliofanywa na walimu na wanafunzi wa VETA.
Katika maonesho ya Sabasaba, VETA ilitembelewa na wananchi 16,072 wakati katika maonesho ya Nanenane Kitaifa kwenye uwanja wa John Mwakangale, Jijini Mbeya, wananchi 7,700 walitembelea katika banda la VETA.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema idadi kubwa ya watu waliotembelea mabanda ya VETA wakati wa maonesho na kutaka taarifa za mafunzo yanayotolewa na vyuo vya VETA nchini ni ishara wazi kwamba wananchi wanatambua umuhimu wa mafunzo hayo katika kuwajengea watanzania ujuzi na kuwawezesha kuajirika na kujikwamua kiuchumi.
“Tunajisikia furaha sana kuweza kutembelewa na wananchi zaidi ya 16,000 kwenye banda letu na kuwahudumia …ushindi tuliopata umetupa nguvu zaidi ya kuendelea kuwahudumia watanzania kwa kuwapatia mafunzo bora ya ufundi stadi,” alisema wakati akizungumzia idadi kubwa ya wananchi waliotembelea banda la VETA kwenye Maonesho ya Sabasaba.
Licha ya kuhitaji taarifa za mafunzo ya ufundi stadi, wananchi wengi wamekuwa wakivutiwa na ubunifu wa teknolojia mbalimbali ambazo zinagusa changamoto mbalimbali katika jamiii.
Katika maonesho ya Sabasaba yaliyofanyika tarehe 28 Juni hadi 13 Julai chini ya kaulimbiu “Tanzania: Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji”, miongoni mwa ubunifu uliokuwa kivutio zaidi kwa watembeleaji wa maonesho hayo ni mfumo wa kielektroniki wa kusaidia watu wenye mahitaji maalum kujihudumia wenyewe, mashine ya kuzidua unga wa ubuyu, mashine ya kufungasha vimiminika, mafunzo ya mapishi na uhudumu wa hoteli, huduma ya ufundi wa simu za mkononi bila malipo, vifaa vya umwagiliaji, mashine za kutengeneza na kuchaganya vyakula vya mifugo, samani za aina mbalimbali na ubunifu wa nguo na mavazi.
Kwa upande wa maonesho ya Nanenane, miongoni mwa teknolojia zilizovutia watu wengi ni madawa ya kuua magugu na wadudu waharibifu mashambani, mashine ya kuchekecha maziwa kupata siagi, mashine ya kukamua mafuta ya karanga na parachichi na teknolojia za kurutubisha udongo.
Katika maonesho ya Sabasaba, mvuto wa ubunifu wa teknolojia, programu za mafunzo na huduma katika banda la VETA ni miongoni mwa sababu zilizoifanya VETA kushika nafasi ya pili katika kundi la Uendelezaji Ujuzi. Mshindi wa kwanza kwenye kundi la Uendelezaji Ujuzi ni Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na nafasi ya Tatu ilichukuliwa na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, alisema ushindi huo umetoa hamasa kwa VETA kuendelea kuboresha zaidi utoaji mafunzo ya ufundi stadi na kuendeleza ubunifu na teknolojia mbalimbali ili kuvutia zaidi uwekezaji na kukuza biashara nchini.
Mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na fursa za kutoa mafunzo kwa madereva 206 wa magari makubwa kutoka kampuni za World Oil Tanzania Ltd, Bravo Tanzania Ltd na Jambo Freight Tanzania Ltd kupitia Chuo cha VETA Kihonda na kutambuliwa na Chama cha Waokaji Tanzania kwa ubunifu wa bidhaa za mbaazi na kitarasa za Chuo cha VETA Njiro na kuahidi kutangaza bidhaa hiyo.
Miongoni mwa viongozi waliotembelea Banda la VETA ni pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein A. Kattanga na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Comrade Abdulrahman Kinana ambao waliipongeza VETA kwa kuwa na teknolojia nzuri za ubunifu wa hali ya juu.
Maonesho ya Sabasaba yalifunguliwa rasmi na Katibu Mtendaji wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AFCFTA), Mhe. Wamkele Mene tarehe 3 Julai 2022, na kufungwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango. Makampuni, Taasisi na Mashirika 3,200 ya ndani na nje ya nchi yalishiriki kwenye maonesho hayo.
Kwa upande wa maonesho ya Nanenane kitaifa, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ndiye aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa ufunguzi, tarehe 1 Agosti 2022 na katika kilele cha maonesho hayo, tarehe 8 Agosti 2022, Mheshiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifunga rasmi maonesho hayo.