The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Kamati ya wataalam wa mawasiliano toka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) leo, tarehe 1 Februari 2024 imefanya ziara kwenye ofisi za VETA Makao Makuu jijini Dodoma kwa lengo la kujifunza na kufahamu fursa mbalimbali zinazotolewa na VETA
VETA baada ya wasilisho lake imeonekana yapo maeneo mbalimbali ambayo JWTZ kwa upande wake linaweza kunufaika nayo. Miongoni mwa maeneo mahsusi yaliyopendekezwa kufikiriwa juu ya ushirikiano ni mafunzo kwenye eneo la mawasiliano, ufundi wa kielektroniki na urasimishaji ujuzi wa fani mbalimbali kwa wanajeshi ambao wamejifunza ujuzi ndani ya JWTZ.
Kiongozi wa ujumbe kutoka JWTZ ambaye ni Afisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Mawasiliano Jeshini, Luteni Kanali Lukwaro Mbwambo aliyemuwakilisha Mkurugenzi wa Mawasiliano Jeshini amesema, JWTZ hutoa mafunzo ya aina mbalimbali jeshini hivyo VETA inaweza kufanya utaratibu wa kuwatambua mafundi wa JWTZ na kurasimisha ujuzi taaluma walizonazo kwa kuwatunuku vyeti.
Amesema kuwa ziara yao VETA imelenga kujifunza na kufahamu fursa za kimafunzo upande wa mawasiliano zinazotolewa na VETA, ambapo jeshi linaweza likanufaika.
“VETA tunajua mnatoa kozi mbalimbali zinazohusu masuala ya mawasiliano ndio maana hasa Jeshi kupitia kamati hii ikaja kujifunza. Tumejifunza mambo mengi ambayo yamekuwa yakiendeshwa ndani ya VETA na mengine hatukuwa tukiyafahamu kuwa yanafanyika VETA,” amesema Luteni Kanali Mbwambo.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Mzee Kasore, ambaye ni Mkurugenzi wa Fedha VETA, amesema kuna maeneo kadhaa ambayo VETA wanaweza kushirikiana na JWTZ na kuleta tija kwa pande zote mbili na Taifa kwa ujumla. Aidha, Bw. Kasore amesema VETA ikiwa ni taasisi ya Serikali inaweza kushirikiana na Jeshi katika nyanja mbalimbali ikiwemo mafunzo ya uzalendo kupitia JKT. Bw. Kasore aliiomba kamati kuwasilisha ombi la kuandaliwa programu maalumu kwa ajili ya kuwaongezea uzalendo watumishi wa VETA ambao hawajapitia mafunzo ya JKT,
CPA Kasore ametaja eneo lingine kuwa ni mafunzo yanayotolewa VETA na yale mafunzo yanayotolewa na JWTZ ambapo yanaweza yakaendeshwa kwa ushirikiano, sambamba na VETA kufanya urasimishaji wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo.
“tunatarajia kuwa na ushirikiano ambao mwisho wa siku utafanya Taasisi hizi kuwa na umoja na ushirikiano utakaowasaidia wananchi wa Tanzania katika maeneo mbalimbali ya kiutendaji, mawasiliano na mengine ya kiufundi,” amesema CPA Kasore.