The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA kuimarisha ushirikiano na Mkoa wa Geita utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi
Posted on: Tuesday, 21 September 2021
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Rosemary Staki Senyamule kwa lengo la kuimarisha utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi mkoani humo.
Mazungumzo hayo yamefanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, tarehe 20 Septemba, 2021 na yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ngazi ya Mkoa, wakiwemo Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita na Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoani humo. Kwa upande wa VETA, kikao hicho kimehudhuriwa pia na Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali na Utawala Bw. Felix Staki, Kaimu Mkurugenzi wa Fedha Bw. Anthony Kasore, Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Ziwa Bw. Charles Kangele na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi Bi. Witness Mgimba.
Katika kikao hicho, viongozi hao wamejadili mambo mbalimbali yanayohusu fursa za mafunzo ya Ufundi Stadi mkoani humo, Maonyesho ya Teknolojia za Uchimbaji Madini yanayoendelea mjini Geita, Matayarisho na ushiriki wa VETA kwenye Wiki ya Vijana inayotarajiwa kufanyika Chato, Mkoani Geita mwezi ujao, na hatma ya Mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Geita uliokwama kutelezwa tangu mwaka 2019 baada ya Serikali kuvunja mkataba kati yake na Mkandarasi aliyekuwa akitekeleza mradi huo, kampuni ya Skywards Construction Co. Ltd.
Kupitia mazungumzo hayo, Mhe. Senyamule ameitaka VETA kushirikiana kwa karibu na ofisi yake kwenye utekelezaji wa majukumu hayo muhimu kwa Mkoa huo na Taifa kwa ujumla, ikiwemo miradi mbalimbali inayotekelezwa na VETA katika mkoa wa Geita.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Bujulu, amemhakikishia Mkuu huyo wa Mkoa kuwa VETA itatoa ushirikiano wa karibu kwa ofisi yake katika kuhakikisha wananchi wa Mkoa huo wanapata ujuzi katika stadi mbalimbali, hasa kwenye Sekta ya madini, kwani Sekta hiyo imebeba sehemu kubwa ya uchumi wa Mkoa huo na wakazi wake.