The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA KUSHIRIKIANA NA YUNIVESO KUZALISHA WAHITIMU MAHIRI
Posted on: Friday, 25 October 2024
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeingia ushirikiano na Kampuni ya YUNIVESO kwa lengo la kushirikiana katika nyanja mbalimbali ili kuwezesha mafunzo na kuwajengea umahiri wanafunzi na wahitimu wa ufundi stadi nchini.
Hati ya makubaliano ya ushirikiano huo imesainiwa na pande zote mbili, tarehe 24 Oktoba 2024, kwenye ofisi za VETA Makao Makuu, Jijini Dodoma.
Hati ya makubaliano inataja lengo kuu la ushiriano kuwa ni kuimarisha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kupitia uandaaji na utekelezaji wa mitaala, uandaaji maandiko na utekelezaji wa miradi kwa pamoja, kubadilishana utaalamu na uzoefu katika utoaji, ugharamiaji na ukuzaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Akizungumza baada ya zoezi la utiaji saini, Mtendaji Mkuu wa YUNIVESO, Bi Fatma Mshinda amesema miongoni mwa mchango wa YUNIVESO katika ushirikiano huo ni kuwawezesha wahitimu wa VETA kupata uatamizi ili kujijenga kiujasiriamali,na kuwatafutia fursa za kushiriki matamasha mbalimbali ili waweze kuelezea shughuli zao na kuweza kumudu ushindani kitaifa na kimataifa.
“Sisi hatuna utaalamu wa kutoa mafunzo, hivyo kazi ya kutoa mafunzo itabaki kwa VETA na sisi tutawawezesha wahitimu kutoka VETA kupata ajira na fursa mbalimbali,” Bi Fatma ameongeza
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA. Anthony Kasore amesema Kupitia makubaliano hayo, itasaidia vijana wa Kitanzania kupata ujuzi utakaowezesha kujiajiri na kuajiriwa, hivyo kupunguza tatizo la ajira nchini.
YUNIVESO ni kampuni ya Kitanzania inayojishughulisha na utoaji ushauri wa kimkakati, kusaidia uendelezaji shughuli za taasisi na ujasiriamali nchini.