The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA MPANDA QUEENS YATINGA LIGI DARAJA LA KWANZA NETIBOLI TAIFA
Posted on: Wednesday, 08 November 2023
VETA MPANDA QUEENS YATINGA LIGI DARAJA LA KWANZA NETIBOLI TAIFA
Timu ya mpira wa pete ya Chuo cha VETA Mpanda, VETA MPANDA QUEENS imeingia hatua ya ligi daraja la I Taifa baada ya kupata ushindi katika mashindano ya ligi daraja la II ngazi ya Taifa kwenye mechi iliyochezwa katika uwanja wa shule ya sekondari Nsimbo,wilayani Mpanda mkoani Katavi.
Akifunga mashindano hayo tarehe 5 Novemba, 2023, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mhe. Jamila Yusuf, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Katavi, alipongeza washindi wa mashindano hayo na kushuruku Chama cha Mpira wa Netiboli Tanzania (CHANETA) kwa kufanya michuano hiyo kufanyika kwenye Mkoa wa Katavi.
Alisema michuano la ligi ratiba ya ligi Daraja la I Taifa yanayotarajiwa kufanyika kati ya mwezi Juni na Julai, 2024, yatahusisha zaidi ya timu tisa(9) kutoka mikoa mbalimbali nchini, ambazo ni pamoja na timu ya UWASA-Mbeya, Bandari ya Dar es Salaam, Mapinduzi Dodoma, Polisi Manyara,Suma JKT (Katavi), Singida Cluster, Mbeya Unity, Njombe na VETA Mpanda Queens.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Netiboli Tanzania (CHANETA) Bi. Rose Mkisi, amesema mashindano hayo yamefungua fursa ya kuibuliwa kwa vipaji vipya vya michezo ambavyo vilikuwa havijulikani nchini kutoka mkoa wa Katavi, huku ikitengeneza mahusiano mazuri kati ya Mkoa wa Katavi na mikoa mingine nchini hasa iliyoshiriki michuano hiyo.
Awali kabla ya kufuzu kuingia Ligi daraja la I Taifa, timu ya VETA-Mpanda Queens ilishiriki mashindano ya ligi daraja la II Taifa yaliyofanyika tarehe 5 Oktoba, 2023 katika viwanja vya shule ya Sekondari Nsimbo-Mpanda mkoani Katavi na kushika nafasi ya tisa ikitanguliwa na timu za Bandari ya Dar es salaam walioshika nafasi ya Kwanza, Mapinduzi Dodoma walioibuka mshindi wa pili, UWASA-Mbeya mshindi wa tatu,Suma JKT(Katavi) mshindi wa nne, Singida Cluster mshindi wa tano, Polisi Manyara mshindi wa sita, Mbeya Unity mshindi wa saba ,Njombe RRH mshindi wa nane na VETA-Mpanda Queens walioshika nafasi ya tisa baada ya kuifunga timu ya Tiger Ladies magoli 95 kwa 52.
Akiongea kwa niaba ya VETA Mpanda Queens, Kocha wa timu hiyo Bi. Isabela Matipa amesema mbali na timu yake kuingia ligi daraja la I Taifa, mashindano hayo yametumika kutangaza fursa za mafunzo ya ufundi stadi zinazopatikana katika chuo cha VETA Mpanda.
“Pamoja na kujenga afya zetu, kufahamiana na kushirikiana na jamii inayotuzunguka na wengine wanaoshiriki mashindano haya, tunafurahi kwamba tumeitumia fursa hii kuendelea kukitangaza chuo chetu hasa kuwajulisha kuhusu kozi tunazozitoa,” amesema.
Tarehe ya michuano ya ligi daraja la I Taifa, pamoja na viwanja ambavyo michuano hiyo itafanyika vitatangazwa mwazoni mwa mwezi Januari, 2024.