The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA na EACOP zasaini makubaliano kutoa ujuzi kwa vijana kushiriki ujenzi wa Bomba la Mafuta
Posted on: Friday, 15 September 2023
VETA na EACOP zasaini makubaliano kutoa ujuzi kwa vijana kushiriki ujenzi wa Bomba la Mafuta
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na kampuni ya Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP Limited), tarehe 14 Septemba 2023, wametia saini Randama ya Makubaliano (MoU) kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vijana wa Kitanzania ili kuwaandaa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki.
Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki linajengwa kwa ajili ya kuyasafirisha mafuta hayo kutoka Hoima, nchini Uganda ambako yanazalishwa, hadi Chongoleani, bandari ya Tanga, nchini Tanzania, ambako yatauzwa kwenye masoko mbalimbali ulimwenguni. Ni bomba la urefu wa kilometa 1,443 ambapo 80% ya urefu wake iko Tanzania.
Hafla ya utiaji saini imefanyika katika hoteli ya Coral Beach jijini Dar es Salaam, ikiwahusisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, na Mkurugenzi Mwendeshaji wa EACOP Limited, Martin Tiffen, kwa niaba ya taasisi zao. Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na maafisa waandamizi kutoka VETA na EACOP.
Akizungumza kuhusu ushirikiano, CPA Anthony Kasore, amesema, “Makubaliano haya yanabainisha fursa kubwa kwa vijana wetu kupata stadi zenye manufaa, kuwawezesha kuajirika, hususani katika mradi wa bomba la mafuta ghafi na kwenye maeneo mengine ya kiuchumi nchini. Ni fursa pia kwetu (VETA) kuongeza nguvu katika juhudi zetu za kufikia dira yetu ya kuwa na Tanzania yenye mafundi stadi mahiri na wa kutosha ili kushiriki katika maendeleo ya nchi kiuchumi na kijamii"
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa EACOP Limited, Martin Tiffen, amesema, ushirikiano huo ni muhimu katika kuwezesha kufikia matokeo mazuri ya mradi.
“kwa kufanya kazi pamoja, tutahakikisha kuwa vijana wa Tanzania wameandaliwa vyema ili kunufaika na fursa zinazotokana na bomba la mafuta ghafi.” Amesema.
Akizungumza kuhusu mpango wa mafunzo, Meneja wa Ajira na Mafunzo wa EACOP Limited, Laurent Stephane amesema, mafunzo hayo yataendeshwa kwa awamu, kwa kuanza na miezi sita ya mafunzo ya stadi za msingi yatakayotolewa kwenye chuo cha VETA Moshi, yakifuatiwa na mafunzo ya miezi sita tena ya umahiri katika fani yatakayotolewa na Taasisi ya Mafunzo ya Petroli Kigumba Uganda (Uganda Petroleum Institute Kigumba-UPIK), kisha mafunzo kwa vitendo sehemu za kazi.
Alisisitiza umuhimu wa kuwanoa vyema vijana ili kuhakikisha wanatambua na kutekeleza viwango na mahitaji ya ufundi katika kazi ya ujenzi wa bomba la mafuta.
“Kufanya kazi katika bomba la mafuta si kazi ya kawaida makosa hayakubaliki unatakiwa kufikiri vyema kabla ya kutenda. Kwa hiyo muwafundishe vijana kutambua na kuendana na misingi ya kazi hiyo,” amesema.
Mafunzo yatakayotolewa kupitia ushirikiano huu yatakuwa na manufaa makubwa kwa maendeleo ya vijana na uchumi wa nchi. Vijana watakaoshiriki katika mafunzo hayo watapata ujuzi unaohitajika katika sekta ya mafuta na gesi, ambayo ni sekta yenye uwezo mkubwa wa kuchochea ukuaji wa uchumi na kutoa ajira.
Kwa mujibu wa Randama ya Makubaliano, miongoni mwa mambo ambayo EACOP itaisaidia VETA katika mradi huo ni pamoja na kuipatia vifaa vya mafunzo katika karakana, kuwezesha walimu wa VETA kupata mafunzo ya kuwaimarisha zaidi na kutoa wataalamu wabobevu katika masuala ya mafuta na gesi ili kusaidia katika mafunzo.
Ushirikiano kati ya VETA na EACOP pia utaleta faida za kiuchumi na kijamii kwa vijana wa Kitanzania.
Vijana watakapopata mafunzo na kushiriki katika ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki, watapata ajira na fursa za kiuchumi, ambazo zitawawezesha kuboresha maisha yao na kuchangia katika maendeleo ya jamii zao