The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA YAANZISHA RASMI UTOAJI MAFUNZO KWA WAFANYAKAZI WA NDANI
Posted on: Tuesday, 09 April 2024
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) inatarajia kuanza rasmi kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa ndani katika vyuo vyake nchini.
Utoaji mafunzo hayo unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Aprili, 2024 baada ya kukamilika kwa mtaala wa mafunzo hayo ulioandaliwa na VETA kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Community Volunteers for the world (CVM) la nchini Italia, kupitia Mradi wa Kuwajengea Uwezo Wafanyakazi wa Majumbani.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya mtaala na mihtasari ya mafunzo hayo jijini Dodoma, leo, tarehe 8 Aprili, 2024, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Antony Kasore amesema mafunzo hayo yataanza kutolewa katika vyuo vya VETA vya Iringa, Dodoma, Mikumi,Tanga, Dar es Salaam na Lindi.
CPA Kasore amesema mafunzo hayo yalianza kwa majaribio katika vyuo vya VETA Mikumi na Dodoma mwezi Januari, 2023 baada ya kuonekana kwa uhitaji wa kuwajengea uwezo wafanyakazi wa majumbani ili watekeleze kazi hizo kwa ufanisi.
Amesema VETA itatumia mtaala huo kuzalisha wafanyakazi wenye ujuzi na vyeti kama ilivyotarajiwa, ambapo itatoa nafasi kwa wafanyakazi hao kufanya kazi kwa kujiamini na ufanisi zaidi na kushukuru CVM kwa ushirikiano walioutoa.
“Tunaishukuru CVM kwa kushirikiana nasi katika uandaaji wa mtaala huu na tunatarajia kwamba tutashirikiana zaidi, lakini pamoja na ushirikiano huo tunafikiria kuwa na wakala ambaye atakuwa daraja la kuwaunganisha wafanyakazi wa ndani na soko la ajira pindi wamalizapo mafunzo,” alisema.
Naye Afisa Mkuza Mitaala kutoka VETA na mratibu wa mradi huo, Anna Nyoni amesema mafunzo kupitia mtaala huo yatafundishwa katika maeneo makuu matatu ambayo ni utunzaji wa watoto, utunzaji wa wazee na wafanyakazi watakaofanya kazi nje ya nchi.
Amesema mafunzo hayo yanatarajiwa kutolewa kupitia kozi za muda mfupi kuanzia mwezi mmoja hadi miezi sita kutegemeana na uhitaji na aina ya mfanyakazi anaetarajiwa kupata mafunzo hayo.
Pamoja na maandalizi ya mtaala, tayari walimu 12 wamejengewa uwezo wa kuweza kutoa mafunzo katika vyuo hivyo.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa CVM, Giovanni Bagna amesema, mbali na kusaidia kuandaa mtaala na mihtasari, shirika lake litasaidia kutoa mikopo nafuu kwa wafanyakazi wa ndani watakaoonesha na nia na uhitaji wa kupata mafunzo na baadae kurejesha kwa utaratibu utakaowekwa ili kuwawezesha wafanyakazi wa majumbani wengi zaidi kunufaika na mafunzo hayo.
“Utekelezaji wa mtaala huu kupitia VETA utatupa nguvu ya pamoja katika kuhakikisha kwamba wafanyakazi hao wanapatiwa mafunzo stahiki hasa katika kipindi hiki tunaposubiri uthibitisho wa kuundwa kwa sheria na Bunge la Tanzania itakayounga mkono tamko namba 189 la Shirika la Kazi Duniani (ILO), linalohitaji kuwekwa kwa mazingira bora na rafiki ya ufanyaji kazi kwa wafanyakazi wa majumbani,” Bagna amesisitiza.