The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA YAINGIA MAKUBALIANO NA TAMA, AMSHA, MIBOSI, RUATI KATIKA KUWAJENGEA UWEZO VIJANA 4870
Posted on: Friday, 28 February 2025
VETA YAINGIA MAKUBALIANO NA TAMA, AMSHA, MIBOSI, RUATI KATIKA KUWAJENGEA UWEZO VIJANA 4870 SEKTA YA KILIMO
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeingia makubaliano na taasisi nne kwa ajili ya kuwajengea uwezo vijana 4870 katika maeneo matatu ya zana na mitambo ya kilimo, umwagiliaji na uhifadhi wa mazao baada ya kuvunwa.
Makubaliano hayo yamefanyika leo tarehe 28 Februari 2025 VETA makao makuu jijini Dodoma.
Akizungumza katika utiaji Saini wa makubaliano hayo Mratibu wa mradi huo Mhandisi Joseph Kimako amesema mradi huu utaanza kutekelezwa katika vyuo vinne vya VETA ambavyo ni Kihonda, Manyara, Arusha na Mpanda ambapo baadae mradi huu utaongeza wigo na kufikiamikoa 18 hapa nchini.
“Vijana wapatao 4870 watanufaika moja kwa moja kwenye mradi wa kujengewa ujuzi lakini pia walimu katika vyuo ambapo maradi utapita watanufaika kwa kujengewa uwezo kwenye fani zao pamoja na jinsi ya kufundisha watu wenye mahitaji maalumu kabla ya kuanza kufundisha ili wawe mahiri nakuwa saidia hao vijana kupata ujuzi wa kutosha” Amesema mhandisi Kimako.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu CPA Anthony Kasore amesema ushirikiano baina ya VETA na taasisi hizo una lenga kuwasaidia wananchi kuweza kujiajiri au kuajiriwa hasa katika sekta ya kilimo, kwa kuwa VETA imekuwa ikitoa mafunzo katika fani ya zana za kilimo.
“VETA imekuwa ikitoa mafunzo kulingana na mahitaji ya eneo husika katika eneo la kilimo ujuzi unahitajika nasisi tunatoa mafunzo huko, hivyo ushirikiano huu una utaimarisha zaidi sekta hii ya kilimo” Amesema CPA Kasore.
Naye Mkurugenzi wa taasisi ya AMSHA Omary Mwaimu,amesema kwa kushirikiana na VETA watajikita katika kuwafundisha vijana kufanya kilimo cha biashara badala ya kulima kilimo cha kawaida amabacho hakina tija.
Nao Mkurugenzi wa TAMA Pascal Nchinda na Dkt Kessam Maswaga Mkurugenzi wa RUATI wameishukuru VETA kwa kukubali kushirikiana nao katika kuwapatia vijana ujuzi hasa katika sekta ya kilimo hapa nchini.
Utekelezaji wa mradi huu ni wa miaka miwili kuanzia 2025 hadi 2027 ambao umelenga kujumuisha wananchi wote katika kupata ujuzi.