The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imejipanga vyema kuhakikisha watanzania wengi zaidi wananufaika na mafunzo bora ya ufundi stadi yanatolewa kupitia vyuo vyake nchini kote.
Akitoa salamu za mwaka mpya kwa Watanzania jijini Dodoma tarehe 4 Januari, 2023, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, alisema kwa mwaka 2023 VETA imedhamiria kuongeza fursa zaidi za mafunzo ya ufundi stadi kwa watanzania ili kuwawezesha kujipatia ujuzi utakaowawezesha kushiriki kikamilifu kwenye shughuli mbalimbali za uchumi.
CPA. Kasore ametaja baadhi ya matarajio ya Mamlaka hiyo kuwa ni kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 90,000 kwa mwaka 2022 hadi 118,000 kwa mwaka 2023 na kumalizia ujenzi wa vyuo 25 vya ufundi stadi vya Wilaya pamoja na kuratibu ujenzi wa vyuo vipya 64 vya Wilaya na chuo cha Mkoa wa Songwe.
“Tumejipanga vyema kuhakikisha kuwa ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vya Wilaya 63 nchini na ujenzi wa chuo cha ufundi stadi na huduma cha Mkoa wa Songwe unatekelezwa kwa ufanisi… Tunashukuru Serikali imeshatenga shilingi bilioni 100 katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya kuanza ujenzi huo,” alisema.
Akizungumza kuhusu mafanikio yaliyopatikana mwaka 2022, CPA Kasore alitaja baadhi ya mafanikio kuwa ni pamoja na kukamilisha kwa asilimia 97 ujenzi wa vyuo 25 vya Wilaya kwa kutumia nguvu kazi ya ndani yaani “Force Account” na uratibu wa ujenzi wa vyuo vinne vya Mikoa ya Simiyu, Njombe, Geita na Rukwa.
Katika kuhakikisha mafunzo ya ufundi stadi yanatolewa kwa ubora, CPA Kasore alisema katika mwaka 2022, jumla ya mitaala 48 ilihuishwa ili kuendana na mahitaji halisi ya soko la ajira na kuakisi mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Aidha, CPA Kasore alisema VETA imeendeleza ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuwafikia watanzania wengi zaidi wenye mahitaji ya mafunzo ya ufundi stadi na kukidhi mahitaji ya makundi mbalimbali kwenye jamii.
Alitaja baadhi ya wadau hao kuwa ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu kupitia mradi wa Uwanagenzi ambapo jumla ya vijana 3900 walipatiwa mafunzo na Shirika la Maendeleo ya Ujerumani (GIZ) kupitia mradi wa E4D kutoa mafunzo kwa vijana 4200 nchini. Wanufaika wote hao walipatiwa mafunzo hayo bila malipo.
CPA Kasore alitoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa kipaumbele kikubwa kwenye elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili kuhakikisha watanzania wanajipatia ujuzi utakaowawezesha kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuwezesha vijana kujiajiri.
“Mhe. Rais amekuwa na malengo makubwa sana katika kuhakikisha elimu ya ufundi stadi inaimarika na kutolewa ndani ya nchi na tumeshuhudia mengi yakifanyika kwenye eneo la kuboresha miundombinu inayotumika kutoa mafunzo ya ufundi stadi… Tunamshukuru sana,” Amesema
Kwa mujibu wa CPA Kasore, moja ya changamoto inayoikabili Mamlaka hiyo ni kushindwa kuhimili idadi kubwa ya watanzania wanaoomba nafasi za kupata mafunzo ya ufundi stadi kwenye vyuo vya VETA ambayo anaamini itatatulia kwa kiasi kikubwa na ujio wa vyuo vya Wilaya na Mikoa, huku Mamlaka hiyo ikiendelea kubuni njia mbadala za utoaji mafunzo kwa watanzania.