The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA yatengeneza mashine za kuchuja mafuta ya Alizeti
Posted on: Friday, 18 August 2023
VETA yatengeneza mashine za kuchuja mafuta ya Alizeti
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kupitia ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Ukuzaji Viwanda (UNIDO) imetengeneza mashine za kuchuja mafuta ya alizeti, kwa lengo la kusaidia wajasiriamali kuongeza ubora wa mafuta hayo.
Mashine hizo zilizotengenezwa na chuo cha VETA Dodoma zimezinduliwa tarehe 17 Agosti, 2023 na jMkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda, kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Wilson Lugano kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Dkt. Lugano amesema, mashine hizo zimefungwa katika viwanda vidogo vya wilaya za Kongwa na Dodoma, zitatoa fursa kwa wasindikaji kwenda kujifunza kwa vitendo namna ya kuchuja mafuta ya alizeti kwa lengo la kuongeza thamani ya mafuta hayo.
Dkt. Lugano amebainisha kuwa mafuta ya kupikia ni bidhaaa muhimu sana inayotugusa maisha ya watu wengi katika jamii ndio maana serikali imeweka msukumo katika uzalishaji wa bidhaa hiyo hapa nchini na kulinda wazalishaji wa ndani.
"Serikali inaagiza zaidi ya asilimia 60 mahitaji yanayotumika hapa nchini, hivyo kubuniwa kwa mashine hizi kutawezesha wasindikaji kuongeza wigo katika kuzalisha mafuta na hivyo kupunguza uagizaji wa bidhaa hii nje ya nchi" Ameongeza.
Kwa upande wake Afisa Mfawidhi kutoka Shirika la Kimataifa la kukuza Viwanda (UNIDO), Gerald Runyoro amesema mashine hizo tatu zimegharimu zaidi ya million 53 mpaka kukamilika kwake.
Amesema gharama ya kuagiza mtambo mmoja nje ya nchi inagharimu zaidi ya shilingi million 40 hivyo kutengenezwa kwa mashine hizo ndani ya nchi kumeipunguzia serikali gharama za kuagiza nje ya nchi ambapo fedha hizo zitatumika kwa shughuli nyingine za maendeleo.
Amesema, wasindikaji wengi wanaoagiza mashine nje ya nchi wamekuwa wakipata changamoto ya mafundi pale mashine zao zinapoharibika, hivyo kutengenezwa kwa mashine hizo katika vyuo vya VETA hapa nchini kutakuwa kumewasaidia wasindikaji hao.
Kwa kupitia kutengenezwa kwa mashine hizi hapa nchini tutakuwa tumeongeza ujuzi lakini pia kwa vijana wetu watakuwa wamepata ajira," amesema.
Naye kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema lengo la kubuni mashine hizo ni kusaidia wajasiriamali na wachakataji wa mafuta ili waweze kutoa mafuta yenye ubora unaohitajika katika soko la ndani ya nchi na nje ya nchi.
CPA Kasore ameongeza kuwa Mtambo mmoja unatengenezwa hapa nchini kupitia VETA kwa Shilingi za Kitanzania mil 17.9, hivyo kuongeza unafuu na urahisi wa kupat mashine hizo.
"Kupatikana kwa mitambo hiii hapa nchini kutasaidia kwa wazalishaji wa mafuta kununua mashine hizi hapahapa nchini na kupunguza uagizaji wa mitambo nje ya nchi kwa gharama kubwa," Amebainisha CPA Kasore
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wasindikaji wa Mafuta ya Kupikia Tanzania (TASUPA), Ringo Iringo amesema uwezo wa mashine hiyo ni mkubwa katika kuzalisha mafuta na gharama yake pia ni nafuu, hivyo wasindikaji wengi watamudu gharama za kununua.
Alipendekeza mitambo hii kuwekwa katika Vituo mbalimbali vya VETA na SIDO hapa nchini ili wasindikaji waweze kwenda kupata huduma katika vituo hivyo.