The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Vijana 4000 kunufaika na mafunzo ya ufundi stadi kupitia mradi waE4D
Posted on: Wednesday, 16 November 2022
Jumla ya vijana 4,000 katika mikoa ya Lindi, Manyara, Dodoma , Dar es salaam wanatarajia kunufaika na mafunzo ya ufundi Stadi kwenye fani za Ufundi Bomba wa Viwandani, Uchomeleaji na Mekatroniki kwenye vyuo vya VETA kupitia mradi wa Ajira na Ujuzi kwa Maendeleo ya Afrika(E4D).
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa vya kufundishia iliyofanyika kwenye chuo cha VETA Lindi tarehe 10 Novemba 2022, Mratibu wa mradi wa E4D Ndugu Kabogo Mbuyi amesema mradi huo unalenga kukuza ujuzi na kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana nchini.
Amesema mradi huo unatekelezwa kupitia Shirika la maendeleo la Ujerumani (GIZ) pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira, na Wenye Ulemavu na unafadhiliwa na GIZ kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Misaada na Maendeleo la Korea KOICA kwa gharama ya shilingi bilioni 1.3.
Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa VETA, Ndugu Felix Staki, ambaye alikuwa akimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa VETA, alisema utekelezaji wa mradi wa E4D utachangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza udahili, kutoa fursa zaidi kwa vijana kupata ujuzi kupitia mafunzo ya ufundi stadi, kuimarisha ubora wa mafunzo ya ufundi stadi kupitia vifaa vya kisasa vya kufundishia pamoja na kuongeza ujuzi kwa walimu wa ufundi stadi.
Alisema katika chuo cha VETA Lindi mradi huo unatarajia kunufaisha vijana 700 watakaopata mafunzo ya muda mfupi kwenye fani za Ufundi Bomba pamoja Uchomeleaji na Uungaji vyuma ambapo jumla ya shilingi 228 milioni zimetumika kununulia vifaa.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bi Zainab Telack, alisema ni matarajio ya Serikali ya Mkoa kuwa vijana watakaohotimu mafunzo hayo watakuwa na ujuzi wa kutosha utakaowawezesha kujiajiri.
Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA Lindi, Ndugu Harry Mmari, alishukuru GIZ kwa vifaa vilivyotolewa ambavyo vitasaidia kutoa mafunzo na kutengeneza ajira kwa vijana .