The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
WABUNGE WAIASA VETA KUJIIMARISHA ZAIDI ILI KUBEBA MAONO YA RAISI SAMIA KUHUSU ELIMU UJUZI
Posted on: Friday, 29 March 2024
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameiasa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kujiimarisha zaidi na kuongeza ubunifu katika utoaji wa mafunzo, kwani inategemewa sana katika kubeba maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhusu elimu ujuzi.
Wakizungumza jana tarehe 28 Machi 2024 baada ya kukagua Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Ikungi, wabunge hao ambao ni wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), wamesema Rais anataka kuona Watanzania wengi wana ujuzi unaowawezesha kuajirika, kuendesha maisha yao na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa Taifa.
“Ukitaka kupima maono ya kiongozi, angalia matendo yake, angalia anakoelekeza rasilimali za nchi. Ukimuangalia Mheshimiwa Rais (Dkt. Samia Suluhu Hassan), utaona kuwa rasilimali nyingi anazielekeza kwenye elimu na amekuwa akisisitiza juu ya Watanzania kuwa na ujuzi,” amesema Mheshimiwa Japhet Hasunga, Mbunge wa Vwawa na Makamu Mwenyekiti wa PAC.
Amesema kuwa VETA ina nafasi kubwa ya kutafsiri kwa vitendo maono ya Rais na kufanya mabadiliko makubwa katika kuwezesha kuinua uchumi wa nchi, kupunguza tatizo la ajira na kuongeza tija viwandani.
“Sera ya CCM ni uchumi wa viwanda. Sera ya viwanda inahitaji ujuzi, tumeliona hili kwa kujenga VETA kila wilaya. Kwa hiyo VETA mna uwezo wa kuibadilisha nchi kwa kiasi kikubwa,” ameongeza.
Sambamba na kuimarisha mafunzo, Hasunga ameishauri VETA kuhamasisha ubunifu ili kuwezesha walimu na wanafunzi kutengeneza bidhaa bora na zinazokubalika kwenye soko.
Kwa upande wake, Mbunge wa viti maalum, Mheshimiwa Janeth Masaburi ameishauri VETA kutafuta fursa za ushirikiano na taasisi za nje ya nchi ili kuwezesha kupata walimu wenye umahiri katika fani mbalimbali ambao watasaidia kuwafundisha na kuwaimarisha walimu wa VETA katika maeneo ambayo wana upungufu wa maarifa kutokana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.
Mbunge Bakar Hamad Bakar kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar ameshauri kufanya juhudi kubwa katika ununuzi wa vifaa bora na vya kutosha kwa ajili ya utoaji mafunzo, sambamba na kufuatilia vibali vya kuajiri walimu wa kutosha kwenye vyuo vya VETA ili utoaji wa mafunzo uwe bora na wa ufanisi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mheshimiwa Thomas Apson amesema VETA sasa inategemewa kuwa mkombozi wa vijana kutokana na changamoto ya upatikanaji wa ajira, kwani tofauti na zamani ambapo Serikali ilikuwa ndio tegemeo kubwa la ajira kwa vijana, sasa mwajiri mkuu ni sekta binafsi ambako ujuzi ndio unatakiwa zaidi.
Akitoa maelezo ya kisera na mikakati ya Serikali katika kuhakikisha wananchi wengi wanapata elimu-ujuzi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Caroline Nombo amesema Sera mpya ya Elimu inasisitiza elimu-ujuzi ambapo hata mitaala mipya ya elimu ya sekondari imeingiza mafunzo ya ujuzi kwa kutumia mitaala ya VETA.
Katika kuimarisha mafunzo kwa vitendo kwenye vyuo vya VETA, Prof. Nombo amesema sasa kuna utaratibu wa mafunzo unaohusisha mafunzo ya sehemu za kazi ambayo yanasaidia kuongeza umahiri wa wanafunzi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VET Board), Prof. Sifuni Mchome amewashukuru wabunge kwa imani yao kwa VETA na kusema kuwa wataendelea kuisimamia VETA na kuhakikisha kuwa utoaji wa mafunzo unaendana na dhana ya uhitaji kwenye soko la ajira.