The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
WALIMU VETA WANOLEWA KUIMARISHA UTOAJI MAFUNZO SEKTA YA NGUO NA MAVAZI
Posted on: Wednesday, 27 March 2024
Walimu 56 wa fani ya Ushonaji, Ubunifu na Teknolojia ya Nguo kutoka vyuo vya VETA nchini wamepatiwa mafunzo yenye lengo la kuwajengea uwezo katika kuboresha utoaji mafunzo, kufuatia mabadiliko ya mitaala katika fani hiyo.
Akifunga mafunzo hayo ya siku tatu yaliyofanyika katika ukumbi wa chuo cha VETA Dodoma, leo tarehe 27 Machi, 2024, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Antony Kasore amesema mabadiliko makubwa yamefanyika katika mitaala ya fani hiyo iliyohuishwa mwaka 2022, ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira.
“Kupitia mafunzo haya, tunatarajia mkawe mawakili wema katika kuhakikisha kwamba ufundishaji unaendana na mabadiliko mitaala na kasi mabadiliko makubwa ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira kwa ujumla” amesisitiza.
Sambamba na kuwajengea uwezo katika eneo la mafunzo, CPA Kasore ameahidi kuwa Mamlaka itafanya juhudi za kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kuwapatia mashine na vifaa vya kisasa vyenye uwezo wa kubeba uhalisia wa mahitaji ya kasi ya mabadiliko ya teknolojia katika ufundishaji.
“wito wangu kwenu baada ya mafunzo haya na mara mtakapopokea vifaa na mashine hizo mtatusaidia kuwaandaa wanafunzi na wahitimu watakaotangaza ubora wa fursa ya mafunzo katika fani, hasa eneo la ubunifu, kujitangaza, kutafuta na kuchangamkia soko kupitia mitandao mbalimbali, pamoja na kuwashirikisha wataalamu kutoka nje ili wanafunzi wetu wahitimu wakiwa wenye tija zaidi”amesema
Akisoma risala kwa niaba ya walimu hao kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Bi.Winifrida Ndunguru kutoka chuo cha VETA-Dakawa amesema, Mafunzo hayo yamewawezesha kupitia changamoto zote zilizokuwa zikiwakabili hasa kwenye eneo la mitaala mipya na kuzipatia ufumbuzi wenye uwelewa wa pamoja,kujifunza mbinu mpya za kupakua mawasilisho kwa njia ya elektroniki, kutumia TEHAMA na mifumo ya mitandao mbalimbali itakayowawezesha kupata zana za kufundishia na kujifunzia kwa nadharia na vitendo na kuahidi utekelezaji wake mara watakaporejea vituoni mwao.
Nae Bi. Anna Nyoni aliemwakilisha Mkurugenzi wa mafunzo VETA Makao Makuu, amemshukuru Kaimu Mkurugenzi Mkuu, kwa kuruhusu na kuona haja ya kuwepo kwa mafunzo hayo ambayo yamefungua njia ya kutolewa kwa ufafanuzi wa mitaala ya kozi hiyo iliyohuishwa mwaka 2022 pamoja na utekelezaji wake.