The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
WALIMU WA VETA WAJENGEWA UWEZO UTEKELEZAJI WA MIONGOZO YA ELIMU JUMUISHI
Posted on: Tuesday, 07 February 2023
Walimu 16 wa ufundi stadi kwenye vyuo vya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wamepatiwa mafunzo juu utekelezaji wa miongozo ya kuboresha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa watu wenye mahitaji maalum nchini.
Akifungua warsha kwa walimu hao katika chuo cha VETA Dodoma leo tarehe 6 Februari, 2023, Kaimu Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa VETA, Ndg. Abdallah Ngodu, amesema miongozo hiyo inalenga kuweka mazingira wezeshi ya kujifunzia na kufundishia watu wenye mahitaji maalum wanaojiunga na mafunzo mbalimbali kwenye vyuo vya VETA.
Amesema idadi ya watu wenye mahitaji maalum wanaojiunga na vyuo vya VETA nchini inaendelea kuongezeka siku hadi siku na kwamba VETA imeona umuhimu wa kutoa kipaumbele kwenye kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa elimu ya ufundi stadi na kuhakikisha walimu wanaelewa vyema mbinu za ufundishaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Kwa mujibu wa Ndg. Ngodu, VETA iliandaa miongozo miwili ambapo mwongozo wa kwanza unaelekeza namna ya kuwajumuisha watu wenye mahitaji maalum kwenye mafunzo kuanzia hatua ya kuwatambua hadi kuwaingiza kwenye kozi na mwongozo wa pili unaainisha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji ambao walimu watautumia kuwafundisha watu hao bila kuwabagua.
“Tunatoa mafunzo kwa walimu ili waweze kuielewa vyema miongozo hii na kuitumia kutoa mafunzo na kuhakikisha watu wenye mahitaji maalum wenye kuhitaji mafunzo ya ufundi stadi kwenye vyuo vyetu wanayapata kwa ufanisi ili yawasaidie kwenye maisha yao,” amesema
Afisa Mkuza Mitaala wa VETA, Bi .Happiness Salema, amesema msisitizo uliowekwa katika miongozo hiyo ni kuwajumuisha watu wenye mahitaji maalum kupata mafunzo pamoja na wasiokuwa na mahitaji maalum na kuweka miundombinu ya kuwawezesha watu hao kujifunza bila vikwazo.
Naye Mkufunzi Mwandamizi wa Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro, Ndg. Rodgers Sabuni, amesema kupitia miongozo hiyo walimu wa vyuo vya VETA wataweza kuwahudumia vizuri zaidi wanafunzi wenye mahitaji maalum tofauti na walivyokuwa wakifanya awali ambapo wengi wao walitumia uzoefu.
Mwalimu wa fani ya Useremala katika Chuo cha VETA Dar es Salaam, Ndg. Salehe Omari amesema mafunzo yaliyoanza kutolewa yamempa fursa ya kufahamu zaidi kwa utaalamu namna ya kuhudumia watu wenye mahitaji maalum na kwamba miongozo iliyoandaliwa itasaidia kuongeza idadi ya walimu wengi zaidi wa kutoa mafunzo hayo.
Naye mwalimu wa Fani ya Mapishi katika Chuo cha VETA Mbeya, Ndg. Asibatike William amesema kupitia mwongozo huo VETA itaweza kuweka mazingira rafiki zaidi ya kufundishia watu wenye mahitaji maalum na kuwajengea ari walimu ya kujiamini zaidi katika kuhudumia wanafunzi hao.
Warsha ya kuwajengea uwezo walimu wa VETA juu ya mbinu za ufundishaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum awamu ya kwanza inajumuisha walimu kutoka katika vyuo vya VETA wa fani za Useremala, Uungaji na Uchomeleaji Vyuma, Ushonaji, Ufundi Umeme, TEHAMA, Mapishi na Utengenezaji wa Bidhaa za Ngozi. Warsha hiyo inafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 6 hadi 8 Februari, 2023.