The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Wanafunzi wa VETA wang’ara katika Mashindano ya Kitaifa ya Ujuzi
Posted on: Sunday, 02 June 2024
Wanafunzi wa VETA wang’ara katika Mashindano ya Kitaifa ya Ujuzi
Wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali vya VETA wametawala Mashindano ya Kitaifa ya Ujuzi mwaka huu ambapo wameibuka washindi kwa nafasi za kwanza hadi tatu katika mashindano hayo yaliyofanyika tarehe 30 na 31 Mei, 2024, jijini Tanga.
Mashindano hayo yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Popatlal yalihusisha wanafunzi 25 kutoka vyuo mbalimbali vya ufundi stadi katika fani za ufundi Uashi, Ufundi Umeme, Mekatroniki, Sanaa ya Mapishi pamoja na Uungaji na Uundaji vyuma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) amewakabidhi zawadi za ushindi washindi hao, tarehe 31 Mei, 2024, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu.
Mwanafunzi Ibrahimu Simba kutoka chuo cha VETA Kihonda ameibuka mshindi wa kwanza katika fani ya Uashi na kufuatiwa na Ramadhani Hussein wa chuo cha VETA Tanga na wa tatu ni Shaban Hamdani wa chuo cha VETA Tanga.
Katika fani ya Ufundi Umeme, Omari Hussein wa Chuo cha VETA Kihonda ameibuka mshindi wa kwanza akifuatiwa na Silvester Mngo'ngo wa chuo cha Almakhtoum College of Engineering na wa tatu ni Goodluck Justine wa chuo cha VETA Kipawa.
Mfungo Sebastian wa chuo cha VETA Kipawa ameibuka mshindi wa kwanza kwenye fani ya Mekatroniki na kufuatiwa na Godwin Justine wa chuo cha VETA Dodoma na wa tatu ni Ester Fabian wa chuo cha VETA Kipawa.
Katika fani ya Uungaji na Uundaji Vyuma, Ramadhani Rajabu wa Chuo cha VETA Tanga ameibuka mshindi wa kwanza akifuatiwa na Ivon Ngonyani wa chuo cha VETA Mikumi na wa tatu ni Jonas Makongo wa chuo cha VETA Tanga.
Hamisa Rashidi kutoka chuo cha VETA cha Hoteli na Utalii ameibuka mshindi wa kwanza kwenye fani Sanaa ya Mapishi na kufuatiwa na Prudence Kirori wa chuo cha VETA cha Hoteli na Utalii na wa tatu ni Haruna Jumanne kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha.
Washindi wa kwanza wamekabidhiwa zawadi ya fedha taslimu kiasi cha Tshs Milioni moja , washindi wa pili shilingi laki nne na wa tatu kiasi cha shilingi laki mbili.
Mashindano hayo ni miongoni mwa shughuli zilizokuwa zikifanyika katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yaliyoanza tarehe 25 Mei, 2024, ambapo kilele chake kilikuwa tarehe 31 Mei, 2024.