The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Wananchi Mbarali waanza kunufaika na mafunzo ya ufundi stadi
Posted on: Monday, 21 November 2022
Wananchi wilayani Mbarali mkoa wa Mbeya wameanza kunufaika na mafunzo ya ufundi stadi katika chuo kipya cha VETA wilayani humo, ambapo tayari wananchi 35 wamehitimu mafunzo ya muda mfupi katika chuo hicho.
Hafla ya kukabidhi vyeti wahitimu hao katika fani za Uashi na Udereva imefanyika tarehe 19 Novemba 2022 ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Ndugu Missana Kwangura amewatunuku vyeti.
Mafunzo hayo yametolewa kupitia jitihada za Mkurugenzi huyo za kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Mbarali wanapata stadi zinazohitajika Wilayani hapo katika kufanikisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Wahitimu hao walipatiwa mafunzo kwa mwezi mmoja kuanzia tarehe 21 Septemba hadi 21 Oktoba, 2022 ambapo wananchi 27 kati yao walifundishwa udereva na nane uashi.
Msimamizi wa chuo hicho ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha VETA Mbeya, Mhandisi Hassan Kalima, amesema kwenye fani ya uashi wananchi hao wamefundishwa kutengeneza tofali bora za saruji kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya Serikali wilayani hapo.
Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Mbarali ni miongoni mwa vyuo vipya 25 vilivyojengwa na VETA kwa kutumia nguvukazi ya ndani (Force account). Chuo hicho kinatarajia kuanza kutoa mafunzo ya muda mrefu mwezi Januari, 2023 katika fani za Ushonaji, Umeme wa Majumbani pamoja na Uhazili na Kompyuta.