The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Wanawake wachangamkia fursa Ujenzi wa Chuo cha VETA Wilaya ya Chamwino
Posted on: Thursday, 06 April 2023
Wanawake katika kijiji cha Mlowa Bwawani, Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma wamejitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa ya maandalizi ya kuanza kwa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, ujenzi ambao kwa sasa upo katika hatua za awali za kupanga majengo na uchimbaji wa msingi.
Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chamwino ni sehemu ya mradi mkubwa wa ujenzi wa vyuo 64 vya ufundi stadi vya wilaya na kimoja cha Mkoa wa Songwe unaotekelezwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Akizungumza leo, tarehe 5 Aprili 2023, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa chuo hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Dkt. Franklin Rwezimula, amewapongeza wananchi wa kijiji hicho, hasa wanawake kwa kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa za maandalizi ya awali ya Ujenzi wa chuo.
Amesema, tofauti na maeneo mengine ambapo wanaume wanakuwa wengi, katika eneo hilo, wanawake wamekuwa wengi kuliko wanaume.
Rwezimula ametoa wito kwa wanaume kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa za ujenzi wa chuo hicho kama walivyofanya wanawake.
“Wananchi pia wanashiriki kwa wingi katika ujenzi wa hiki chuo katika kutoa nguvu kazi, nihamasishe wananchi wa kata hii wajitokeze kwa wingi waje wafanye kazi, Kazi hizi sio za bure zinalipwa, malipo watakayopata katika kazi hizi zitawasaidia kuinua uchumi wa kaya zao pamoja na uchumi wa kata,” amesema.
“Nimefurahi kuona washiriki wengi ni akina mama kama mnavyojua akina mama ndio wanatunza familia wanachokipata kinaenda kutunza watoto lakini nihamasishe akina baba pia wasibaki nyuma mje mshiriki, mama akikusanya na wewe ukakusanya mkachanganya kinakuwa kikubwa”.
Kwa mujibi wa Dkt. Rwezimula, chuo hicho kitatoa kozi ambazo zitawezesha vijana wa Chamwino kujipatia ujuzi kwenye fani mbalimbali na kuweza kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Dkt. Rwezimula alimshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pesa ambazo zitajenga vyuo vya VETA 64 nchi nzima.
Diwani wa Kata ya Mlowa ndugu Andrew Mseya amemhakikishia Dkt. Rwezimula ushiriki wa wananchi wake kwenye ujenzi huo na usalama wa vifaa vya ujenzi vitakavyoletwa kwa ajili ya ujenzi.
Mkuu wa kitengo cha Sheria VETA, Bi.Dora Mweta akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa VETA, ametoa wito kwa wananchi wa Mlowa Bwawani kuona ujio wa chuo hicho kuwa ni kwa manufaa yao na kwa sababu ya kuthaminiwa na Serikali, hivyo wajitokeze kwa wingi kujitolea katika Ujenzi.
Ameongeza kuwa ujenzi wa chuo hicho utaongeza ukuaji wa eneo hilo, kwani kutavutia maendeleo ya mji huo, kutaleta mabadiliko mengi kutaleta ikiwemo umeme, maji na huduma zingine za kijamii.