The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
WASIMAMIZI WA VYUO VYA VETA KANDA YA KATI WAJENGEWA UWEZO KUIMARISHA UTOAJI MAFUNZO YA UFUNDI STADI
Posted on: Wednesday, 03 July 2024
WASIMAMIZI WA VYUO VYA VETA KANDA YA KATI WAJENGEWA UWEZO KUIMARISHA UTOAJI MAFUNZO YA UFUNDI STADI
Wasimamizi wa vyuo vya VETA Kanda ya Kati wamepewa mafunzo ya kuwajengea uwezo katika kuimarisha utoaji mafunzo ya ufundi stadi.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na uongozi wa VETA Kanda ya Kati, yametolewa kwa Wasimamizi hao kutoka vyuo tisa vilivyopo katika kanda hiyo ambavyo ni vya VETA Dodoma, Manyara, Singida, Kongwa, Bahi, Chemba, Ikungi, Simanjiro na chuo cha VETA-Gorowa yamefanyika tarehe 1 Julai, 2024 katika ukumbi wa Serengeti uliopo katika kituo cha Mikutano cha Mt. Gasper jijini Dodoma.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Antony Kasore amewahimiza wasimamizi hao kufanyia kazi yale yote yaliyoelekezwa ikiwa ni pamoja na kuzingatia maadili ya msingi ya VETA yanayomtaka kila mtumishi kuwajibika katika nafasi yake katika kuwezesha utoaji wa Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini.
“sisi ndio watatuzi wa masuala yahusuyo ufundi katika maeneo tunayoyaongoza, hivyo mafunzo haya yakawasaidie kutekeleza wajibu wenu kwa kufanya kazi kwa pamoja, kwa ufanisi, kwa ubunifu mkiwa na mawasiliano sahihi, mkiwasilikiza na kuwasaidia Watanzania wenye uhitaji wa ujuzi katika ufundi stadi kupitia mafunzo mtakayoyatoa,” alisisitiza.
Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati, Ramadhani Mataka amesema mafunzo hayo yametoa fursa kwa wasimamizi wa vyuo vya VETA Kanda ya kati, kujadili na kukubaliana kwa pamoja juu ya namna bora ya kuimarisha utoaji mafunzo, kuongeza udahili wa wanafunzi katika vyuo vyao na kutengeneza mazingira wezeshi ili kuwasaidia wasimamizi hao kuhakikisha kwamba wanatekeleza wajibu wao kwa ufanisi na weledi.
“kupitia mafunzo haya kajiwekeeni usimamizi na utaratibu mzuri wa kufanikisha utekelezaji wa utoaji mafunzo kwa kuwa ndicho kipimo kitakachoonesha uwajibikaji wetu uliotukuka,”amesema
Nae Kaimu Mkuu wa chuo cha VETA cha Mkoa wa Manyara, Bi. Nansanga Godwin, ameushukuru uongozi wa VETA Kanda ya Kati kwa kuandaa mafunzo hayo na kuahidi ushirikiano wa kutosha katika kuyatekeleza yale waliyojifunza na maagizo yaliyotolewa.
Mafunzo hayo yamehusisha jumla ya wasimamizi 53 wakiwepo Wakuu wa vyuo vya VETA Kanda ya Kati, Wasajili, Mameneja Rasilimali watu, Mameneja Ununuzi, Wahasibu, Wakuu wa Idara za Uzalishaji pamoja na Makatibu Mahsusi kutoka VETA Kanda ya kati.