The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Watumishi VETA Makao Makuu wafundishwa kukabiliana na majanga ya moto
Posted on: Monday, 20 June 2022
Watumishi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Makao Makuu wamepatiwa mafunzo ya namna mbalimbali za kukabiliana na kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ya moto.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, tarehe 16 Juni 2022 kwenye ofisi za VETA Makao Makuu, jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema kuwa uongozi umeamua kutoa mafunzo hayo kwa watumishi ili waweze kufahamu tahadhari wanazopaswa kuchukua kuepuka majanga ya moto na njia sahihi za kukabiliana na moto pindi unapotokea.
“Mafunzo haya ni muhimu sana kwetu wafanyakazi kwa kuwa yanatusaidia kujenga ufahamu wa namna tunavyoweza kuzuia majanga ya moto, lakini pia kukabiliana na moto pale unapotokea tukiwa ofisini na hata majumbani kwetu,”amesema CPA Kasore.
Amewataka watumishi hao kufanyia kazi mafunzo waliyoyapata ili kuepusha majanga ya moto ambayo yanaweza kuzuilika na kuepusha madhara yanayotokana na moto.
Kwa upande wake Afisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji jijini Dodoma, SSGT. Joyce Kapinga, amesema bado kuna watu wengi hawafahamu njia sahihi za kukabiliana na majanga ya moto kutokana na ukosefu wa elimu juu ya aina za visababishi vya moto na namna ya kukabiliana na moto pale unapotokea.
“Watu wengi wanaathirika na majanga ya moto kwa kushindwa kukabiliana na moto hasa ukiwa kwenye hatua za awali, badala yake moto husambaa na kuleta madhara makubwa… naamini baada ya mafunzo haya watumishi wa VETA watakuwa mabalozi wazuri kwa watu wengine wa namna ya kukabiliana na majanga ya moto,” amesema SSGT. Kapinga.
Mafunzo hayo yaliyotolewa kwa njia ya nadharia na vitendo yamehusisha watumishi 85 wa VETA Makao Makuu kutoka idara mbalimbali.