The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Watumishi VETA waaswa kutoa huduma bora kuendana na kasi ya ukuaji wa Taasisi
Posted on: Monday, 27 February 2023
Watumishi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), wameaswa kuimarisha utoaji wa huduma kwa wateja ili kuendana na kasi ya ukuaji na kupanuka kwa Mamlaka hiyo.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa VETA Ndg, Felix Staki, wakati akifungua semina ya Utoaji wa Huduma Bora kwa Wateja iliyowahusisha watumishi wa mapokezi wa VETA, tarehe 22 Februari, 2023.
Amesema VETA inaendelea kupanuka zaidi ambapo inachangiwa pia na kuendelea kwa ujenzi wa vyuo vipya katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo kuzidi kuongezeka kwa wateja wanaohitaji huduma zake.
Amesema ongezeko la watu wanaohitaji huduma za VETA linatakiwa kwenda sambamba na uboreshaji wa utoaji huduma ili wananchi wengi zaidi wanufaike na elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
Amesema eneo la mapokezi ni eneo muhimu sana kwenye Taasisi yoyote kwa kuwa lina mchango mkubwa katika kujenga au kubomoa taswira ya Taasisi na kusisitiza umuhimu wa watumishi wa mapokezi kutekeleza kazi zao kwa weledi.
“Shughuli za utoaji mafunzo zinazofanywa na Mamlaka yetu zinaendelea kupanuka siku hadi siku na vyuo vinaendelea kuongezeka… Tunatakiwa kujipanga vyema kutoa huduma bora kwa kundi kubwa la watu wanaoendelea kufika kwenye vyuo vyetu kupata huduma mbalimbali zinazohusiana na elimu na mafunzo ya ufundi stadi,”amesema
VETA inamiliki vyuo 49 vinavyotoa mafunzo ya ufundi stadi katika fani mbalimbali ambapo vyuo hivyo vinatarajiwa kuongezeka hadi kufikia 73 ifikapo mwisho wa mwaka 2023 kutokana na ujenzi wa vyuo vya Ufundi Stadi unaoendelea katika Wilaya mbalimbali nchini.
Ndg. Staki amesema utoaji wa huduma bora kwa wateja ni wajibu wa kila mtumishi wa VETA katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa na huduma sahihi kulingana na mahitaji yao.
Katika warsha hiyo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo Huduma za Mapokezi, Mbinu za Kuimarisha Utoaji wa Huduma Bora kwa Wateja, Mkataba wa VETA wa Huduma kwa Wateja na Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma.
Jumla ya watumishi wa mapokezi 20 kutoka vyuo mbalimbali vya VETA wameshiriki semina hiyo iliyofanyika katika Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi (MVTTC) mjini Morogoro tarehe 22 hadi 23 Februari, 2023.