The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) CPA. Anthony Kasore, amewapongeza watumishi wa VETA kwa utendaji wa kazi mzuri katika mwaka wa fedha 2023/2024 na kupelekea VETA kupata ‘Hati Safi.’
CPA Kasore ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na watumishi wa VETA Makao Makuu, katika kikao cha watumishi, kilichofanyika leo, katika ukumbi wa Chuo cha VETA Dodoma, tarehe 23 Agosti 2024.
CPA. Kasore amesema kuwa katika Mwaka 2023/2024, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imepata mafanikio mengi ikiwemo kupata Hati Safi iliyotokana na ushirikiano na utendaji wa watumishi ikiwa ni pamoja na kusimamia ipasavyo utekelezaji wa malengo ya taasisi kwa ujumla.
Ameainisha baadhi ya mafanikio ambayo VETA imepata ni pamoja na ongezeko la udahili wa wanafunzi kufikia 83,974; kujenga vyuo vipya ishirini na tano (25) kwa kutumia nguvukazi za ndani; kusimamia ujenzi wa vyuo vinne vya ngazi ya mkoa, hivyo vyuo 29 kuanza mafunzo katika maeneo mbalimbali.
CPA Kasore ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa usimamizi thabiti, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyosaidia kwa kiasi kikubwa katika utendaji na kuiwezesha VETA kufikia malengo ya Serikali.
Amesema, Serikali bado inaendelea kujenga vyuo vya ufundi stadi nchini na ifikapo 2025, VETA inatarajiwa kuwa na vyuo 145 na jukumu kubwa la VETA ni kuvisimamia na kuviendesha kwa ubora vyuo hivyo ili viweze kunufaisha vijana kupata ufundi stadi, hatimaye kuajiriwa na kujiajiri
Amewakumbusha watumishi kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anaendelea kuhimiza vijana nchini wapewe mafunzo ya ujuzi, hivyo VETA inatakiwa kuhakikisha inatekeleza ipasavyo maono, nia na dhamira ya Mhe. Rais.
“Tutumie muda wetu katika kutekeleza majukumu yetu kwa kusikiliza sauti ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kama dira yetu”, CPA. Kasore alisisitiza.
Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Mamlaka, Ndugu Eniart Fabian Mahundi, amewakumbusha watumishi kufuata taratibu za Utumishi wa Umma katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.