The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Wawekezaji Sekta ya Madini waelekezwa kufadhili wanafunzi wa ufundi stadi
Posted on: Sunday, 02 June 2024
Wawekezaji Sekta ya Madini waelekezwa kufadhili wanafunzi wa ufundi stadi
Wawekezaji Sekta ya Madini wameelekezwa kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaosoma fani zinazohusu madini katika vyuo vya ufundi nchini ikiwemo vyuo vya VETA.
Maelekezo hayo yametolewa leo, tarehe 24 Mei, 2024 na Naibu Waziri wa Madini, Mheshimiwa Dkt Steven Lemomo Kiruswa, alipokuwa akifunga rasmi Jukwaa la Tatu la Utekelezaji wa Uwezeshwaji wa Watanzania katika sekta ya madini, lililoanza tarehe 22 Mei, 2024 na kufikia kilele leo.
“Nawaelekeza wawekezaji ambao wanataka kujenga viwanda kwa ajili ya kutoa huduma kwenye migodi watoe ufadhili kwa vyuo vya ndani kama VETA ili kuwawezesha vijana wanaoandaliwa kuchukua nafasi katika viwanda vitakavyojengwa na kuwapeleka wakasome nje wale ambao vyuo vitawapendekeza kutokana na uwezo mkubwa watakaouonyesha,” amesema Naibu Waziri Kiruswa.
Naibu Waziri amewaelekeza wawekezaji wenye nia ya kujenga viwanda vitakavyokuwa vikitoa huduma migodini kuhakikisha wanaajiri watu wenye ujuzi, hivyo nguvu kubwa iliekezwe kuwajengea uwezo Watanzania kwa kuanzisha utaratibu wa kubadilishana uzoefu katika mafunzo kutoka kwa wadau wa nje.
“Hivi viwanda vinahitaji watu wenye taaluma ambayo hatuna, tutalazimika kutafuta wadau kutoka nje na wale wadau wanaweza wakaja na Watanzania wakaishia kujifunza tu kwa vitendo bila kupata ujuzi stahiki. Hivyo viwanda hivi vinaweza kutenga mafungu kwaajili ya ufadhili,” amesema.
Sambamba na hilo Naibu Waziri Kiruswa amesema ipo haja ya vyuo vya ndani kufungamanishwa na wenye viwanda ili mahitaji mahsusi yanayotakiwa na hivi viwanda yaendane na mitaala katika vyuo na hata wakati wa uundaji mitaala iendane na mahitaji ya hivyo viwanda.
“Nashauri wenye viwanda kutembelea vyuo na kuangalia aina ya mafunzo yanayotolewa, na mshauri namna ya kuboresha mitaala,” amesema.
Mkurugenzi wa VETA, Kanda ya Kaskazini, Monica Mbele ameishukuru Chemba ya Madini Tanzania kwa kufadhili mafunzo ya IMTT yanayotolewa na chuo cha VETA Moshi.
Sambamba na shukurani hizo amewaomba wadau wa sekta ya madini nchini kuendelea kudhamini mafunzo yanayotolewa na vyuo vya VETA nchini.
Pia ameomba kupatiwa mashine za kisasa zaidi katika vyuo vya VETA ili kuwaweza wanafunzi kupata uhalisia wakinacho fanyika mgodini.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kiruswa amewataka wenye viwanda kutoa fursa kwa wanafunzi wa vyuo kupata sehemu ya kujitolea hata kama hawatawalipa ujira wowote ili waweze kujifunza kwa vitendo kabla ya kupata ajira.
Naibu Waziri ametoa maagizo baada ya hoja iliyoibuliwa katika mjadala na Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Magharibi, Asanterabu Kanza alipokuwa akichangia mjadala katika jukwaa hilo.
Amehitimisha kwa kutoa rai kwa watanzania na wawekezaji katika sekta ya madini kuchangamkia fursa ambazo zimebainishwa kupitia Jukwaa la Tatu la Uwezeshwaji na Ushirkishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, hususani uanzishwaji wa viwanda vinavyohitajika migodini, kwani mahitaji yake ni makubwa nchini.