Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeahidi kusaidia ubunifu wa “Pikipiki Salama” uliofanywa na Mwalimu wa Chuo cha VETA Kipawa, Aneth Mgana ili kuwezesha kuingia katika matumizi.
Ahadi hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu alipotembelea chuo cha VETA Kipawa Alhamisi, tarehe 18 Julai 2019 ili kujifunza zaidi juu ya ubunifu huo.
Meja Jenerali Kingu ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa ubunifu huo akisema kuwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kulinda usalama wa dereva, abiria na watumiaji wengine wa pikipiki ambao wamekuwa wakiathiriwa kwa kiasi kikubwa na ajali za pikipiki.
Alisema Wizara yake ipo tayari kuuwezesha ubunifu huo kuingia katika matumizi na kumtaka mbunifu wa pikipiki hiyo Aneth Mganga kuainisha na kuwasilisha mahitaji yake Wizarani.
Ubunifu uliopo kwenye “Pikipiki Salama” ni wa mfumo unaozuia pikipiki kuwaka endapo dereva hajavaa kofia ngumu (helmet).
Mbunifu pia anapanga kuongeza kipengele cha kuzuia pikipiki kuwaka endapo dereva amelewa pombe, kutoa taarifa endapo dereva amebeba abiria anayetaka kumdhuru na kutoruhusu kubeba abiria zaidi ya uwezo wake, maarufu kama mshikaki.
Aidha Katibu Mkuu huyo alisema kuwa Wizara yake itaishirikisha VETA kwenye mpango wa kuandaa tela maalum itakayofungwa kwenye pikipiki kwa lengo la kusaidia kuepusha ajali na kuongeza kipato kwa waendesha bodaboda.
“Tunahitaji sana utaalamu wa watu wa VETA katika mradi huu tunaoufanya hasa upande wa TEHAMA na hivyo tutahakikisha mnashiriki kikamilifu ili kwa pamoja tuweze kuondoa wimbi la ajali za pikipiki” Alisema
Taasisi zingine zinazohusika kwenye mradi huo ni Shirika la Mzinga, Shirika la Nyumbu, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na Chuo cha Usafirishaji nchini (NIT).
Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu aliongozana na Wajumbe wa Kamati Maalum ya Wataalam ya Udhibiti wa ajali za pikipiki ambao nao walitoa mawazo yao katika kuiboresha pikipiki hiyo ili iweze kuendana na mazingira halisi ya hapa nchini.
Takwimu zinaonyesha kuwa kwa miaka kumi (2009 – 2018) jumla ya watu 35,231 wamejeruhiwa kufuatia ajali za pikipiki huku vifo vilivyotokana na ajali hizo vikiwa ni 8,004.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office