Tarehe 14 Februari ambayo huadhimishwa kama Siku ya Wapendanao (maarufu kama Valentine) imekuwa njema kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwani imeambatana na tukio muhimu la Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani kutoa jumla ya ekari 200 kwa VETA ambalo litasaidia kupanua shughuli za utoaji elimu na mafunzo ya ufundi stadi, hususani kwa vyuo vya VETA vilivyoko Dar es Salaam.
Akizungumza kabla ya makabidhiano ya eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mheshimiwa Jokate Mwegelo alisema ni bahati kubwa kwa VETA kupata eneo hilo ambalo limekaa kimkakati kutokana na kuwa na miundombinu muhimu na kuzungukwa na maeneo muhimu kiuchumi.
Alisema, eneo hilo lililopo kwenye kitongoji cha Kazimzumbwi, kata ya Kazimzumbwi halmashauri ya Kisarawe mji liko kandokando ya barabara inayotoka Kisarawe mjini kwenda kwenye Pori la Hifadhi la Selous ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami na kwamba Reli ya Kati, Standard Gauge na TAZARA pamoja na mradi wa maji kwa ajili ya wilaya ya Kisarawe vyote vinapita eneo hilo.
Vilevile, alisema eneo hilo liko jirani na ukanda maalum wa kiuchumi (special economic zone), ambao unaweza kutoa fursa kwa vijana kupata maeneo ya kufanyia mazoezi ya vitendo na ajira baada ya kuhitimu mafunzo yao.
“Mkoa wa Pwani tumejipambanua kama mkoa wa viwanda. Lakini ili viwanda viwanufaishe vyema wananchi wa Kisarawe kuna mahitaji makubwa kwa vijana kupata ujuzi kwa ajili ya kufanya kazi kwenye viwanda. Kwa hiyo tunaona ni jambo la msingi VETA waje watusaidie kuinua ujuzi kwa vijana na watu wetu. Tunahitaji nguvukazi yenye ujuzi,” alisema.
Alisema, ni matumaini yake kuwa baada ya VETA kukabidhiwa eneo hilo watafanya juhudi za haraka kuanza kuliendeleza.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu aliushukuru uongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kwa kuwa tayari na kwa wepesi kutoa eneo hilo kwani litasaidia kwa kiasi kikubwa kupanua shughuli za mafunzo ya VETA, hususani kwa kanda ya Dar es Salaam.
Alisema, vyuo vya VETA vya Dar es Salaam (Chang’ombe) na Kipawa viko katika maeneo madogo sana ambapo vimejibana na kukosa nafasi za kupanua huduma zao, kwa hiyo kupatikana kwa eneo hilo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupanua mafunzo ya vyuo hivyo.
Alisema, wapo pia wadau ambao wameonesha nia ya kushirikiana na VETA kutoa mafunzo katika maeneo mbalimbali kama kilimo, usafirishaji na TEHAMA lakini jambo la nafasi lilikuwa linaonesha dalili ya kuwa kikwazo.
Aliongeza kuwa eneo hilo linaweza kusaidia hata kujenga mabweni ya wanafunzi wa vyuo vya VETA Dar es Salaam na Kipawa ambavyo vyote viwili havina mabweni, hivyo wanafunzi wote wa vyuo hivyo wanahudhuria mafunzo kwa kutwa.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office