The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Wananchi wa Wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe wanatarajia kuanza kupata mafunzo ya ufundi stadi katika Chuo cha VETA kinachotarajiwa kuanzishwa Wilayani Wanging'ombe katika mwaka wa masomo ujao.
Hayo yamebainishwa tarehe 4 Agosti, 2021 na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, alipotembelea na kukagua majengo na miundombinu katika Kijiji cha Ufwala, ambayo itakarabatiwa na kuboreshwa ili kukidhi mahitaji ya msingi ya chuo cha ufundi stadi.
Dkt. Bujulu amesema Chuo hicho kitaanzishwa katika majengo na miundombinu iliyokuwa ikimilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe kufuatia Halmashauri hiyo kukabidhiwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS). Awali, majengo hayo yalitumiwa na Mhandisi Mkazi aliyesimamia ujenzi wa Barabara ya Nyigo-Igawa, mkoani Njombe.
Kwa mujibu wa Dkt. Bujulu, Halmashauri ya Wilaya ya Wanging'ombe ilikabidhi majengo hayo kwa VETA mwezi Mei, 2020 baada ya wananchi wa Wilaya hiyo kupendekeza majengo hayo yatumike kutoa mafunzo ya ufundi stadi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ufwala kilipo Chuo hicho, Bw. Failos Ng'umbi, amesema kuwa wananchi wa kijiji chake wanasubiri kwa hamu kubwa kuanza kwa mafunzo Chuoni hapo.
Alisema mahitaji ni makubwa mno Wilayani humo, hivyo akaiomba VETA kuharakisha matayarisho, ili mafunzo hayo yaweze kuanza haraka iwezekanavyo. Mwenyekiti huyo amebainisha kuwa kijiji chake kiko tayari kutoa ardhi ya nyongeza kwa kadri ya mahitaji ya VETA kwa ajili ya kupanua Chuo hicho. Kwa niaba ya Mamlaka, Mkurugenzi Mkuu alimshukuru Mwenyekiti na viongozi wengine waliohudhuria ukaguzi huo, wakiwemo Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Wanging’ombe Bw. Erasto Danda, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Wanging’ombe (WEO) Bi. Beth Mangula na Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ufwala (VEO) Bi. Irene Nungwi.