Wajasiriamali na wahitimu wa ufundi stadi nchini wana fursa ya kunufaika na mikopo yenye masharti nafuu baada ya taasisi tano nchini kuungana kwa pamoja kuwezesha wananchi kuanzisha viwanda.
Taasisi zilizounganisha nguvu ni Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na Benki ya Azania, ambazo zimesaini kwa pamoja Makubaliano (MoU) ya kushirikiana kuwawezesha wananchi kuanzisha viwanda vidogo na vya kati.
Makubaliano hayo yametiwa saini tarehe 21 Februari, 2020 na Watendaji Wakuu wa Taasisi hizo katika ofisi za NSSF Makao Makuu, Jijini Dar es Salaam.
Tayari NSSF imetenga jumla ya Shilingi Bilioni Tano (Bil. 5) zitakazotolewa kupitia Benki ya Azania, ambayo ndiyo itakuwa na jukumu la kukopesha wajasiriamali wadogo na wa kati.
Katika makubaliano hayo, VETA na SIDO zitakuwa na jukumu la kuwatambua, kuwajengea uwezo na kuwapendekeza wajasiriamali kwa ajili ya mikopo itakayotolewa kupitia Benki ya Azania.
Vilevile, VETA itakuwa na majukumu ya kusimamia miradi iliyopata mikopo kupitia kwake na kutoa mafunzo na ushauri wa kitaalam kwa wajasiriamali ili kuwasaidia kuboresha miradi yao na kuendesha uzalishaji kwa tija na ufanisi zaidi.
Akifafanua juu ya mikopo na utaratibu wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania, Charles Itembe, alisema kuwa kiwango cha mikopo midogo kitaanzia Shilingi mil. 8 hadi mil. 50 na kiwango cha kati ni kilicho juu ya mil. 50 hadi mil. 500.
Katibu Mtendaji wa NEEC ambayo ndio yenye dhamana ya uwezeshaji wananchi, Bi Beng'i Issa, alisifu makubaliano hayo na kusema kuwa kipaumbele kitatolewa kwa viwanda vya bidhaa ambazo hazipatikani hapa nchini na vile ambavyo vitashirikisha wananchi wengi, kwa kuwa lengo ni kuhakikisha watanzania wengi wanashiriki katika shughuli za kiuchumi.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, alishukuru kuanzishwa kwa ushirikiano huo na kusema kuwa VETA itahakikisha inatoa ujuzi unaostahili kwa wananchi kulingana na viwanda husika na kwamba itasimamia vyema zoezi la kutambua wajasiriamali hao.
Dkt Bujulu amesema “Natoa wito kwa wananchi wenye nia ya kuanzisha viwanda kujitokeza kwa wingi ili kuweza kutambuliwa ili watakaokidhi vigezo waweze kupata mikopo hiyo”.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. William Erio, alisema kuwa muunganiko huo umelenga hasa kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kuhakikisha wananchi wote wanapata fursa ya kushiriki.
Alisema kiasi hicho cha Shilingi Bilioni Tano (Bil. 5) ni kianzio tu ambapo mfuko huo utaweza kuongeza fedha nyingine kulingana na mahitaji na ufanisi wa awamu hii ya kwanza.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office