The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
TIMU YA VETA MAKAO MAKUU YAICHAKAZA SEKRETARIETI YA MAADILI
Posted on: Sunday, 08 September 2024
Timu ya mpira wa miguu VETA Makao Makuu imejinyakulia ushindi wa mchezo baada ya kuiichapa timu ya Sekretarieti ya Maadili goli 4 -3, jana jioni, tarehe 6 Septemba 2024, katika viwanja vya Kilimani, Uzunguni, jijini Dodoma.
Mechi hiyo ya kirafiki imechezwa ikiwa ni ufunguzi wa maandalizi ya ushiriki wa mashindano yatakayoshirikisha taasisi za Serikali – SHIMUTA.
Katika dakika ya Kumi na tisa mchezaji machachari, Christopher Msigwa, aliliona lango la timu ya Sekretarieti ya Maadili kwa mkwaju wa penaiti, na kufungua mlango kwa goli la kwanza.
Dakika ya Thelathini na mbili, Juma Nassari aliwainua tena mashabiki wa timu ya VETA Makao Makuu kwa kutumbukiza goli la pili.
Baada ya mapumziko wachezaji wa VETA Makao Makuu waliendeleza ubabe, ambapo dakika ya hamsini na tano, Julius Mchanake alifunga goli la tatu na dakika ya themanini na sita, Juma Nassari alihitimisha kifurushi ya magoli kwa bao la nne lililoifanya VETA Makao Makuu kumaliza mchezo kifua mbele kwa ushindi.
Baada ya kuisha kwa mchuano huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Francis Komba alipata wasaa wa kuongea na wachezaji pamoja na mashabiki kutoka VETA Makao Makuu aliwapongeza kwa ushindi huo lakini aliwataka kujiandaa na mashindano ya SHIMUTA kwa kufanya mazoezi ili kupata ushindi katika mashindano hayo yajayo.
Mwenyekiti wa Michezo VETA Makao Makuu, Christopher Msigwa alitoa wito kwa wanamichezo kuanza mazoezi ikiwa ni maandalizi ya mashindano ya SHIMUTA.
“Nawataka wanamichezo tufanye mazoezi ili tupate timu bora na ratiba ya kufanya mazoezi itatolewa siku ya Jumatatu, naomba wachezaji wa mpira wa miguu, Netball na kuvuta kamba wajitokeze,” Msigwa alisisitiza.