The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA, ENABEL KUWEZESHA VIJANA KUPATA UJUZI, KUTUNZA MAZINGIRA
Posted on: Tuesday, 20 August 2024
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Shirika la Maendeleo la Ufalme wa Ubelgiji (ENABEL) zimesaini Hati ya Mashirikiano kwa lengo la kuboresha kuwezesha vijana kupata ujuzi na kushiriki katika utunzaji mazingira.
Makubaliano hayo yametiwa saini, tarehe 19 Agosti 2024, katika ukumbi wa Hotel ya Protea, Jijini Dar es Salaam na Wakurugenzi Wakuu wa taasisi hizo.
Makubaliano yatahusisha utekelezaji wa miradi miwili itakayotekelezwa katika vyuo vya VETA Kipawa, Mwanza, Tanga, Kasulu, Kigoma na Buhigwe.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kutiliana saini, Mkurugenzi Mkuu wa Enabel nchini Tanzania, Ndugu Koenraad Goekint alisema, shirika lake limewalenga zaidi vijana wa kike kwa kuwapatia ulinzi na usawa wa kijinsia, kuwapatia elimu na ujuzi na kutafuta fursa za kazi.
“Wasichana na wanawake vijana wenye umri wa miaka 14 hadi 19 watawezeshwa kupata elimu ya ufundi stadi kwa kushirikiana na VETA, kuwatafutia ajira na kuwaongezea fursa za kujiajiri," Koenraad amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, ameitaja miradi itakayotekelezwa ni "Wezesha Binti" na "Elimu ya Utunzaji Mazingira."
Amesema, Wezesha Binti ambao unalenga kuwawezesha mabinti kupata elimu ya Ufundi Stadi ili waweze kuajiriwa na kujiajiri utatekelezwa Kigoma Mjini na Kasulu.
Ameongeza kuwa mradi wa elimu ya kutunza mazingira utatekelezwa katika mikoa ya Tanga na Mwanza na vijana watapewa mafunzo kuhusiana na ujuzi wa kutunza miundombinu ya mazingira na kuweza kushiriki katika shughuli za kiuchumi.