Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yamezinduliwa rasmi tarehe 14 Novemba 2018 huku Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ikipewa jukumu la kuratibu mchakato wa mashindano katika makundi mawili ambayo ni Wabunifu wa Ufundi Stadi na Wabunifu wa kutoka Sekta Isiyo Rasmi, hivyo kupata majina matano ya kila kundi kuingia kwenye fainali.
Akizindua mashindano hayo sambamba na Mwongozo wa Kuendeleza Ugunduzi, Ubunifu na Maarifa Asilia, kwenye Ukumbi wa Kambarage, Nyerere square jijini Dodoma, Waziri wa sayansi na teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema mashindano hayo yataongozwa na kaulimbiu ya “Kukuza Ujuzi na Ubunifu kwa Uchumi wa Viwanda,” na yatahusisha makundi mbalimbali ya wabunifu wa kisayansi, teknolojia katika maeneo na nyanja mbalimbali nchini kote, ambapo kilele chake kitakuwa Januari 2019.
Alisema ili nchi yetu iweze kunufaika na matokeo ya ubunifu, uvumbuzi na maarifa asilia, kuna umuhimu wa kuwahamasisha wagunduzi, wabunifu na wamiliki wa maarifa asilia.
“Kwa hiyo, mashindano haya yatasaidia kuibua vipaji na kuhamasisha uendelezaji wa teknolojia na ubunifu utakaoweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo endelevu ya viwanda, kuongeza tija ya uzalishaji wa malighafi, kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini pamoja na kuboresha shughuli nyingine za kiuchumi. Kutokana na kutambua umuhimu wa sayansi, teknolojia na ubunifu, Wizara yangu ina mpango wa kufanya mashindano haya yafanyike kila mwaka ili uibuaji wa vipaji vya namna hii uwe endelevu, ” alisema.
Aliongeza kuwa Mwongozo wa Kuendeleza Ugunduzi, Ubunifu na Maarifa Asilia utakuwa ni nyenzo ya kuongeza ufanisi wa taasisi zinazoshughulikia masuala ya ugunduzi, ubunifu na umiliki wa maarifa asilia.
Akifafanua juu ya umuhimu wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa maendeleo na ustawi wa taifa Profesa Ndalichako alisema Sayansi, Teknolojia na Ubunifu zimeleta mapinduzi makubwa katika sekta mbalimbali kama vile habari, biashara, viwanda na huduma mbalimbali za kijamii huku akitoa mfano wa mabadiliko katika huduma za kifedha yaliyosababishwa na ubunifu wa matumizi ya teknolojia ya simu za kiganjani.
Alisema mchakato wa mashindano hayo utaratibiwa kwa ushirikiano wa Kurugenzi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH); Taasisi ya Teknolojia (DIT); Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Mashindano hayo yatahusisha jumla ya makundi sita ambayo ni Wabunifu kutoka Shule za sekondari wakiratibiwa na TAMISEMI; Wabunifu wa Ufundi Stadi na Wabunifu wa Sekta Isiyo Rasmi wakiratibiwa na VETA; Wabunifu wa Ufundi wa Kati wakiratibiwa na DIT; na Wabunifu wa Vyuo Vikuu na Wabunifu wa Taasisi za Utafiti wakiratibiwa na COSTECH.
Awali kabla ya kumkaribisha Waziri, Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Daktari Leonard Akwilapo, alitaja malengo mahususi ya mashindano hayo kuwa ni pamoja na Kuibua na kutambua ubunifu mahiri nchini katika eneo la sayansi na teknolojia; Kukuza hamasa ya ubunifu katika nyanja ya sayansi na teknolojia; Kuhamasisha matumizi ya sayansi, teknolojia, ubunifu na hisabati katika shughuli za kiuchumi na kijamii; Kuchochea ugunduzi na ubunifu wa kisayansi na teknolojia utakaotegemeza maendeleo ya uchumi wa viwanda; na Kushirikisha wadau ili kupata mawazo ya jinsi sayansi, teknolojia na ubunifu yanavyoweza kuchangia katika kujenga uchumi wa viwanda.
Alisema wabunifu bora watano kutoka katika kila kundi watachaguliwa katika mchujo wa awali ili kuingia katika mashindano ya fainali yatakayofanyika jijini Dodoma ili kupata washindi watatu wa fainali.
VETA HEAD OFFICE,
12 VETA Road.
41104 Tambukareli,
P.O. BOX 802, Dodoma Tanzania,
Email: info@veta.go.tz
Telephone: +255 26 2963661
Fax: +255 22 2863408
Url: www.veta.go.tz
© 2018 - VETA Head Office