The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Majaliwa akerwa TBA kuchelewesha mradi wa ujenzi na ukarabati wa chuo cha VETA Karagwe
Posted on: Monday, 20 September 2021
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, amesema kuwa amekerwa na ucheleweshaji uliokithiri katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi na ukarabati wa Chuo cha Ufundi stadi cha Wilaya ya Karagwe, unaotekelezwa na Wakala wa Ujenzi Tanzania (TBA).
Akizungumza alipofanya ziara ya kukagua mradi huo tarehe 19 Septemba, 2021, katika Chuo hicho kilicho katika eneo la Kayanga wilayani Karagwe, Mhe. Majaliwa amesema ucheleweshaji huo unakwamisha mpango wa Serikali wa kuboresha chuo hicho kwa kuweka miundombinu ya kisasa, ikiwemo mitambo na zana mpya za kufundishia.
“huu mradi ulitakiwa umalizike mwaka jana lakini mpaka leo bado haujakamilika na nimegundua kwamba TBA ndiye anayekwamisha mradi huu. Bahati mbaya sana kila mahali TBA inalalamikiwa … lazima tukae na Waziri wa ujenzi tuone ni kwa nini TBA kila mradi wanaopewa hawamalizi kazi kwa wakati hata kama fedha zipo.” amesema
Mhe. Majaliwa ameiagiza TBA kuhakikisha inakamilisha mradi huo haraka iwezekanavyo ili kuwezesha wananchi wa Karagwe kunufaika na moboresho yanayogharimiwa na Serikali kwa karibia Shilingi bilioni 6. Amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, kusimamia kwa karibu ukamilishaji wa mradi huo kwa ufanisi.
Amesema mwelekeo wa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwawezesha watanzania kuboresha uchumi wa mtu mmoja mmoja na hivyo ameamua kuwekeza katika kujenga vyuo vya VETA kila Wilaya nchini ili kuwawezesha wananchi kupata ujuzi utakaowaweza kufanya shughuli hizo kwa ufanisi.
“kuna kundi kubwa la watanzania wanaotaka kuingia kwenye shughuli za kiuchumi na njia sahihi ya kuwawezesha ni kuwapa taaluma ya elimu ya ufundi stadi ili kila mmoja awe na ujuzi afanye shughuli yake ya ujuzi itakayomletea tija.” amesema
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga, amesema Wizara yake imekubaliana kukaa na mkandarasi, mshauri elekezi na VETA ili kuweka mkakati wa kukamilisha mradi huo.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi na ukarabati wa chuo hicho, Mshauri Elekezi wa mradi huo Dkt. Ezekiel Moshi wa kampuni ya E.Z.M. Architects & Associates, amesema kazi ya ujenzi inayofanywa na mkandarasi TBA ilianza mwezi Julai, 2018 na ilitarajiwa kumalizika mwezi Julai 2019.
Dkt. Moshi amesema utekelezaji wa mradi huo umekuwa ukisuasua kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa vifaa na hali ya hewa pamoja na udhaifu katika mtiririko wa kifedha (cash flow) kwa upande wa Mkandarasi.
“Ili kumpa nafasi mkandarasi aweze kumalizia kazi hii, amekuwa akiomba muda wa nyongeza kwa muda wa miaka miwili sasa” amesema
Amesema jumla ya majengo nane mapya yanajengwa yakijumuisha Jengo la Utawala lenye Maktaba, Maabara ya “electronics” na Maabara ya Kompyuta, Jengo la maliwato, Jengo la Mafunzo ya ufundi mchanganyiko (Multi-purpose shed), Jengo la bohari (General Store),Jiko na bwalo la chakula, Karakana ya ufundi umeme (Electrical Workshop), Jengo la maliwato ya wasichana na Hosteli ya wavulana huku majengo mengine matano yakifanyiwa ukarabati.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza udahili wa wanafunzi kutoka wanafunzi 160 hadi 320, nafasi ya bweni kwa wanafunzi hususani wanaotoka maeneo ya vijijini na kuboresha utoaji mafunzo kutokana na kununuliwa kwa mitambo na zana mpya za kisasa, kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia ambapo jumla ya shilingi bilioni 1.3 zimetengwa.
Dkt. Bujulu amesema tangu chuo hicho kilipokabidhiwa VETA mwezi Januari, 2021 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, wananchi wa Karagwe wamenufaika na mambo mbalimbali ikiwemo punguzo kubwa la Karo kutoka Tsh. 950,000 hadi Tsh. 120,000 tu kwa mwaka kwa wanafunzi wa bweni na kutoka Tsh.600,000 hadi Tsh. 60,000 tu kwa mwaka kwa mwanafunzi wa kutwa, punguzo lililoanza kutumika tarehe 1 Julai, 2021.
Amezitaja fani zinazotolewa kwenye chuo hicho kuwa ni pamoja na Umeme wa Majumbani, Ubunifu wa mavazi, Ushonaji na Teknolojia ya Nguo, Uchomeleaji na Uungaji vyuma, Ufundi Magari, Uashi, Useremala, Uhazili na Kompyuta pamoja na Elektroniki.