The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA yakabidhi vifaa vya milioni 62 kwa vyuo binafsi
Posted on: Thursday, 12 August 2021
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kupitia VETA Kanda ya Kati imetoa vifaa vya kufundishia vyenye thamani ya Shilingi Milioni 62.8 kwa vyuo vya Ufundi Stadi vinavyomilikiwa na watu binafsi, Mashirika ya Dini na Mashirika ya Kijamaa.
Akikabidhi vifaa hivyo katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma tarehe 3 Agosti, 2021, Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati Bw. John Mwanja amesema uwezeshaji huo unalenga kuboresha utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi katika kanda hiyo, kuongeza udahili na kuwezesha vyuo kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Amesema VETA inatambua mchango mkubwa unaotolewa na vyuo binafsi katika kuwapatia vijana ujuzi na hivyo imeona ni vyema kuviongezea nguvu vyuo hivyo ili viweze kujiimarisha katika kutoa mafunzo.
"Tunaamini kupitia vifaa hivi tulivyovitoa leo utoaji mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi utaenda kuboreka na hatimaye kuandaa vijana wetu ili waweze kuhitimu wakiwa na stadi mahiri zitakazowawezesha kujipatia ajira na kukuza uchumi," alisema
Naye Mratibu wa Vyuo vya Ufundi Stadi Kanda ya Kati, Bi Joyce Mwang’onda, alisema vifaa hivyo vimekuwa vikitolewa kwa awamu na kutaja vyuo vilivyonufaika kuwa ni Don Bosco VTC, St.Gabriel VTC, St.Ursula Ludochowaski, Sema VTC, na Veyula VTC.
Naye mwakilishi wa Mkuu wa Chuo cha Don Bosco Bw. Auson Ntoba alisema vifaa hivyo vitainua hamasa kwa wanafunzi kujifunza kwa vitendo zaidi .
Naye Mkuu wa chuo cha St. Ursula VTC Sista Josephina Mbori aliishukuru VETA kwa msaada huo wa vifaa na kuahidi kuvitumia vyema kutoa ujuzi kwa wanafunzi chuoni hapo.