The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Waziri Ndalichako apongeza utoaji wa mafunzo ya Uanagenzi katika vyuo vya VETA mkoani Kigoma
Posted on: Wednesday, 17 August 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako (Mb), ametembelea vyuo vya VETA mkoani Kigoma na kuonesha kuridhishwa na utoaji mafunzo ya uanagenzi kwa vijana yanayoendeshwa na vyuo mbalimbali vya VETA kwa ufadhili wa Ofisi ya Waziri Mkuu.
Akiwa katika ziara katika vyuo vya VETA Nyamidaho na Kigoma, tarehe 4 na 5 Agosti 2022, Profesa Ndalichako amepongeza walimu kwa kuwawezesha vijana kupata ujuzi katika kipindi kifupi cha mafunzo.
"Nimeona ndani ya miezi miwili mambo ambayo mmeshajifunza ni mambo makubwa sana mtafikiri mnamaliza kesho wakati bado mpo miezi minne, mkimaliza hii miezi minne iliyosalia mtakuwa mko vizuri zaidi, nawapongeza sana. Natoa pongezi zangu kwa wakufunzi wanaotoa mafunzo haya, ukiona vyaelea vimeundwa…Haya mazuri ninayoona kwenu vijana ni kutokana na kazi nzuri inayofanywa na wakufunzi wa VETA...endeleeni kuwapika vijana wetu…hongereni sana," amesema.
Vilevile, Waziri Ndalichako ametumia fursa hiyo kuzitaka halmashauri nchini kutoa kipaumbele kwa vijana wanaohitimu mafunzo ya ufundi stadi chini ya mradi huo wakati wa kutoa mikopo kupitia asilimia kumi ya mapato ya halmashauri ili waweze kuanzisha shughuli zao na kujiajiri, hivyo kusaidia kutatua changamoto za ajira nchini.
Amesema mfuko wa maendeleo ya vijana ambao uko chini ya ofisi ya Waziri Mkuu pia umeboreshwa ili kuongeza wigo wa kutoa mikopo kwa vijana, ambapo pia kiwango kimeongezwa kutoka milioni kumi za awali hadi shilingi milioni 50.
Jumla ya vijana 316 wanapata mafunzo kupitia programu hiyo katika vyuo vya VETA Kigoma na Nyamidaho katika fani za Ufundi Umeme wa Majumbani, Ufundi Umeme wa Magari, Ufundi Bomba, Uashi, Utunzaji na Matengenezo ya Kompyuta, Ufundi wa vifaa vya Kielektronikia, Utengenezaji wa Viyoyozi na Majokofu, Utengenezaji wa vifaa vya Alminium, Uchomeleaji na Uungaji vyuma, Ukarabati wa Bodi za magari na Ushonaji Nguo na Ubunifu wa Mavazi.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Kigoma, Paul Kimenya, amesema kupitia mafunzo hayo ya uanagenzi, chuo kimenufaika kwa kutumia ujuzi wa wanagenzi hao kufanya ukarabati wa baadhi ya miundombinu ya chuo kadiri ya fani walizosomea pamoja na kupata vifaa vya mafunzo katika karakana ambavyo vimesaidia kuboresha mafunzo chuoni hapo.
Jumla ya vijana 7,760 wanaendelea na mafunzo kwa njia ya Uanagenzi katika vyuo 62 vya ufundi stadi nchini, kati yao 3988 wanapata mafunzo hayo kwenye vyuo 30 vya VETA. Mafunzo hayo yalianza mwezi Juni 2022 na yanatarajiwa kumalizika mwezi Desemba, 2022.
Programu ya Kukuza Ujuzi nchini inalenga kuwezesha nguvukazi ya Taifa kupata ujuzi na stadi za kazi stahiki ili kumudu ushindani katika soko la ajira ambapo kwa sasa inatekelezwa kwa awamu ya nne.